BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
SHIRIKISHO la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limepokea barua toka chama cha Soka nchini Zimbabwe (ZIFA) wanakotokea nyota wa Yanga Donald na Thaban Kamusoko kuomba mechi ya kirafiki ya Kimataifa dhidi ya timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itakayofanyika Novemba 13 nchini humo.

Mchezo huo upo kwenye kalenda ya Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA ambapo Stars kama itafanikiwa kuibuka na ushindi ugenini itakuwa imejiweka kwenye nafasi nzuri katika viwango vya ubora vinavyotolewa na Shirikisho hilo kila mwezi.

Ofisa Habari wa TFF Alfred Lucas alisema wamepokea barua hiyo toka ZIFA kuhusu mwaliko huo na wamethibitisha kushiriki kwakua mchezo huo unatambuliwa na FIFA ambao unaweza kuwaipandisha Stars endapo itaibuka na ushindi ugenini.

Lucas alisema Kocha Mkuu wa Stars Charles Boniface Mkwasa anatarajia kutangaza kikosi cha Wachezaji watakaingia kambini kwa ajili ya mtanange huo muda wowote kuanzia sasa.

"Tumepokea barua ya mwaliko kutoka kwa wenzetu ZIFA wameomba mechi ya kirafiki Novemba 13 nasi tumekubali muda wowote kuanzia sasa Kocha Mkwasa atatangaza kikosi kitakachoingia kambini moja kwa moja kwa ajili ya mchezo huo" alisema Lucas.

Wakati huo huo timu ya vijana ya Taifa chini ya miaka 17 'Serengeti boys' wameingia kambini hii leo kwa ajili ya kujiwinda na michuano maalum itakayofanyika Korea Kusini baadae mwezi huu.

Post a Comment

 
Top