BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
DIRISHA dogo la usajili linatarajiwa kufunguliwa keshokutwa Jumanne huku timu mbalimbali za Ligi Kuu ya Vodacom zikiwa kwenye mchakato wa kuboresha vikosi vyao lakini mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel amewaambia viongozi wake kuwa wasithubutu kumtema kipa Vincent Angban.

Gabriel maarufu kama Batgoal ameiambia BOIPLUS kuwa amefuatilia matokeo ya timu yake pamoja na kiwango cha wachezaji wa timu hiyo na kugundua kuwa kipa huyo raia wa Ivory Coast ni kipa bora kwa hapa nchini na kufungwa kwake ni matokeo ya mchezo.Hivi sasa kuna tetesi za kutemwa kwa kipa huyo huku wakitajwa makipa mbalimbali kuziba nafasi yake akiwepo kipa wa African Lyon Youthe Rostand raia wa Cameroon. Hiyo imeelezwa kuwa ni kutokana na Angban kufungwa mabao yanayosemekana kuwa ni mepesi na ya aina moja.

Batgoal alisema kuwa viongozi wa Simba hawana sababu ya kufanya hivyo ila wanapaswa kumtafuta kipa bora zaidi atakayekuwa anabadilishana na Angban ikiwa ni pamoja na kuleta upinzani mkubwa na kuongeza umakini zaidi.

"Hawa naona wanataka kujichanganya sasa, nafuatilia sana mwenendo wa Simba mara nasikia wanataka kumfukuza Angban, je kwa Tanzania hii utapata kipa gani mzuri wa kumzidi Angban. Watulize akili vinginevyo watapotea."Inasikitisha kuona wakati ule anadaka na timu haifungwi hawakumlalamikia Angban sasa hivi wamepoteza mechi mbili ndio wanaona makosa yake, mpira hauendi hivyo, waangalie nafasi ambazo zimepwaya na kuziongezea nguvu kama beki wa kulia na hata kushoto kumsaidia Tshabalala (Mohamed Hussein)," alisema Batgoal.

Simba ilicheza mechi 15 na kwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa pointi 35 huku ikipoteza mechi mbili za mwisho dhidi ya African Lyon walipokubali kipigo cha bao 1-0 na ile ya Prisons waliyofungwa bao 2-1.

Post a Comment

 
Top