BOIPLUS SPORTS BLOG

KOCHA wa zamani wa Simba, Zdravko Logarusic ameishitaki Simba katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa kuvunja mkataba wake na kutaka kulipwa fidia ya dola 40,000 zaidi ya Sh 80 milioni kwa sasa.

Loga alifungua madai hayo kupitia kampuni ya uwakili ya 'Wambilianga Majani and Associates' na kuwataka Simba kulipa fidia hiyo ndani ya siku kumi tangu kutumwa kwa barua hiyo.

Simba wamekiri kupokea barua hiyo ya madai na kwamba wanaifanyia kazi kujua ni jinsi gani wanamalizana na kocha huyo aliyefungashiwa virago tangu Agosti, 2014 nafasi yake ilichukuliwa na Mzambia Patrick Phiri ambaye pia hakuweza kudumu na kikosi hicho kwani alitimuliwa baada ya mechi nane pekee ambazo alitoka sare saba na kufungwa moja.

Wakati wanavunja mkataba wake, Rais Evans Aveva alisema walifikia uamuzi huo baada ya Loga kushindwa kuendana na matakwa na miiko ya klabu huku ikieleza kuwa walijaribu kufanya naye vikao ili kubadilisha mwenendo wa tabia yake ila ilishindika na hivyo kuvunja mkataba wake ikiwa ni miezi mitatu pekee tangu asaini mkataba wa mwaka mmoja. Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele amekiri kupokea barua ya madai ya Loga kutoka FIFA na kwamba wanaifanyia kazi.Simba ilimwajiri Loga ambaye alikuwa na misimamo mikali kwa wachezaji wake hasa kwa wale wasiojituma akitokea timu ya Gor Mahia ya nchini Kenya na ndiye aliyependekeza usajili wa beki Donald Mosoti ambaye Simba walimvunjia mkataba wake saa chache kabla ya dirisha la usajili kufungwa nafasi yake ikichukuliwa na Emmanuel Okwi.

Mosoti pia aliishitaki Simba kwa kosa la kuvunja mkataba wake pasipokuwa na makubaliano yoyote. FIFA iliamuru Simba imlipe Mosoti Sh 64 milioni, fedha ambayo tayari Simba ililipa baada ya awali kushindwa kulipa faini ya dola 14,000 kwa miezi mitatu waliyokuwa wamepewa .

Post a Comment

 
Top