BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
Mohamed Fakih katikati alipokuwa akiichezea Simba, hii katika mechi dhidi ya Mtibwa


BEKI wa zamani wa Simba, Mohamed Fakih anatarajia kusaini mkataba na Kagera Sugar muda wowote kuanzia sasa baada ya mazungumzo ya awali kufanyika.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa kitu pekee kilichobaki ni kusaini mkataba ikiwa ni pamoja na kujiunga na kikosi hicho ambacho kimeingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom unaotarajia kuanza mwezi ujao.

Chanzo hicho kilisema kuwa usajili wa Fakih ni mapendekezo ya kocha wao Mecky Mexime ambaye alikuwa anafanya kwa usiri mkubwa, lengo lake ni kuboresha hasa safu ya ulinzi na inadaiwa kuwepo na mipango pia ya kumnasa kipa Juma Kaseja.Imeelezwa kuwa uongozi wa Kagera Sugar umefanya vikao kwa siku mbili kujadili juu ya usajili wao na tuhuma za wachezaji wanaodaiwa kuhujumu timu yao katika mechi yao na Yanga walipofungwa bao 6-2 tuhuma ambazo zinamhusu kipa Hussein Sharif 'Casillas' aliyesimamishwa na beki Eric Kyaruzi.

Kama uongozi utaamua kuwasamehe wachezaji hao waliosimamishwa basi hawatakuwa na haja ya kusajili kipa mwingine na kama wataachana nao basi watalazimika kuongeza kipa mwingine atakayesaidiana na mkongwe David Burhan.

BOIPLUS ilizungumza na Fakih ambaye alikiri kuwepo kwa mipango hiyo, "Ni kweli tumezungumza na tumefikia pazuri hivyo kila kitu kikiwa tayari kitawekwa wazi zaidi, mimi ni mchezaji na soka ndiyo ajira yangu hivyo sichagua wapi nicheze ninachoangalia ni maslahi tu,".

Post a Comment

 
Top