BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma
 Benno Kakolanya akiwa na kocha wake wa kwanza, Aswile Augustino mjini Sumbawanga

MLINDA mlango wa timu ya Yanga Benno Kakolanya ameenda mjini Sumbawanga mkoani Rukwa kumpelekea zawadi ya vifaa vya michezo Kocha aliyemuibua katika soka, Aswile Augustino ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wake uliomfikisha alipo hivi kwa sasa.

Aswile ambaye ni mlemavu wa miguu alimfundisha Kakolanya kwenye timu yake ya vijana ya Sinza ya huko Sumbawanga baada ya mlinda mlango huyo kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2008 na kumpandisha timu ya wakubwa kabla ya kutimkia Mbaspo Academy ya Mbeya na baadae Makongo ambako Tanzania Prisons walimnyofoa mwaka 2013.

Kakolanya alijiunga na Yanga msimu huu akitokea Prisons ambapo katika mechi mbili za mwisho za kukamisha mzunguko wa kwanza alionyesha kiwango kikubwa baada ya kuokoa penati kwenye mchezo dhidi ya waajiri wake wa zamani Prisons akiwasaidia mabingwa hao watetezi kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye  uwanja wa Sokoine kabla ya kudaka kwenye mchezo wa mwisho walioibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting.


Benno akikabidhi baadhi ya vifaa vya michezo alivyompelekea kocha wake Aswile  

Kakalonya ameiambia BOIPLUS kuwa mshambuliaji Amissi Tambwe ambaye anacheza nae Yanga ndiye aliyekuwa akimuumiza kichwa alipokuwa akiidakia Prisons huku mburundi huyo akifanikiwa kumfunga bao moja pekee na kwa sasa Ibrahim Ajib wa Simba ndiye anayempa mawazo kutokana na umahiri wake anapolikaribia lango la timu pinzani.

"Tambwe anatisha sana nilikuwa nikikutana nae nakuwa makini mno, aliwahi kunifunga bao moja tu kipindi kile lakini kwa sasa namuona Ajib ni mzuri japokuwa hivi karibuni naona kama ameshuka kidogo ila akiwa katika kiwango chake inabidi uwe na uangalifu mkubwa dhidi yake," alisema Kakolanya.

Kipa huyo alisema pia wakati amekubali kujiunga na Yanga watu wengi walimbeza na kumwambia anaenda kukaa benchi kutokana na umahiri wa walinda mlango Deo Munishi 'Dida' na Ally Mustapha 'Bathez' badala yake makipa hao ndio wamekuwa na mchango mkubwa kwake kwavile wanamuelekeza mambo mengi ambayo yanamsaidia.

Post a Comment

 
Top