BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
KIUNGO wa Ndanda FC, William Lucian 'Gallas' amejipanga kurejea kwa kishindo mzunguko wa pili wa ligi kuu baada ya kufutiwa adhabu yake ya kufungiwa mwaka mmoja kwa kosa la kuingia mkataba na timu mbili tofauti.

Shirikisho la Soka nchini  (TFF) lilimfungia Gallas baada ya kubaini alisaini na Mwadui FC ya Shinyanga huku akiwa tayari amesaini mkataba na Ndanda. Hata hivyo TFF ilifuta adhabu hiyo baada ya Gallas kuandika barua ya kuomba msamaha kwa kufanya kosa hilo.

Gallas ameiambia BOIPLUS kuwa baada ya kurudishwa kwenye timu yake hakuweza kuitumikia kwani aliumia goti na sasa yuko vizuri na anaweza kuwemo katika mchezo wao kwanza dhidi ya Simba kwenye mzunguko wa pili wa ligi utakaopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Desemba 17.

"Mzunguko wa pili nitakuwa na Ndanda kwani suala langu lilikwisha,  nimejipanga kurudi kwa kasi ili kuisaidia timu yangu," alisema Galas ambaye alitakiwa kurudisha mshahara wa mwezi mmoja aliokuwa amepewa na Mwadui FC pamoja na gharama ya tiketi ya Ndege alipokuja kuwasilisha barua TFF.

Gallas alisema timu yao haikuwa bora sana mzunguko wa kwanza kutokana na wachezaji wao tegemeo kuwa majeruhi huku mshambuliaji wao nyota Atupele Green akitimkia JKT Ruvu.

"Tuliwakosa Paul Ngalema, Aziz Sibo  na Omari Nyenje huku Atupele akiondoka kwahiyo tulikuwa na mapungufu baadhi ya idara ila mzunguko wa pili tutakuwa bora zaidi," alisema Gallas.

Post a Comment

 
Top