BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
BEKi wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala' kesho Alhamisi anatarajia kwenda kumalizana na klabu hiyo kwa kusaini mkataba wa miaka miwili.

Tshabalala ambaye alisaini Simba mkataba wa miaka mitatu akitokea Kagera Sugar anamaliza mkataba huo mwishoni mwa msimu huu huku akitoa masharti mawili ambayo ni kuboreshewa pesa ya usajili pamoja na mshahara. Mkataba unaomalizika Tshabalala alisaini kwa Sh 4 milioni.

Imeelezwa kuwa Simba wameonyesha nia ya kukubaliana na masharti mapya yaliyotolewa na mchezaji huyo ambapo leo walitaka kumalizana naye ila Meneja wake Herry Mzozo aliutaka uongozi wa klabu hiyo kuwa na subira hadi kesho.

Mzozo ameiambia BOIPLUS kuwa, "Sio kweli kwamba Tshabalala anakwenda Yanga ingawa milango iko wazi ila hakuna timu iliyoleta ofa yake zaidi ya Simba ambao leo wamenipigia simu kuwa tukamalizane.


"Baada ya simu hiyo niliyopigiwa na Hans Poppe nilimweleza baadhi ya mabadiliko ya kimkataba ambayo hayakuwepo kwenye mazungumzo ya mwanzo wameonyesha kukubali maana maisha yanabadilika hivyo mkataba lazima uboreshwe, kesho (Alhamisi) mchana tutakwenda huko, labda washindwe kutoa pesa tuliyowaambia," alisema Mzozo na kuongeza.

"Endapo haya mambo niliyowaleza yatatekelezwa basi hakuna shaka kwamba Tshabalala atasaini Simba hiyo kesho maana ndiyo timu iliyopewa kipaumbele," alisema Mzozo.

Awali meneja huyo aliwaambia Simba waweke Sh 40 milioni mezani ili mchezaji huyo asajiliwe pesa ambayo ipo tayari ila sasa kuna mapendekezo mapya ambayo bado ni siri yao na kama kuna timu itahitaji huduma ya Tshabalala basi ni kufuata kanuni ya kwenda kumalizana na uongozi wake kwa maana ya kuvunja mkataba.

Katika siku za hivi karibuni timu za Yanga na Azam zimetajwa kumuwania beki huyo kipenzi cha wanasimba lakini kwa makubaliano hayo zitakuwa zimebakiwa na masaa machache tu ya kufanya lolote kabla hajafunga 'ndoa' mpya na wekundu hao Msimbazi.

Post a Comment

 
Top