BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
HUKUMU ya kesi ya beki wa Yanga Hassan Ramadhan Kessy inatarajiwa kutolewa Alhamisi Novemba 3 baada ya juzi kushindikana kutokana na Wakili wa Yanga kutoa udhuru.

Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) iliketi juzi chini ya Makamu Mwenyekiti wake Raymond Wawa Oktoba 29 kwa ajili ya kutoa maamuzi ya mwisho lakini Wakili wa Yanga Alex Mgongolwa alipata msiba mkoani Iringa hivyo ikashindikana kusikilizwa.

Simba walimshtaki Kessy baada ya kusaini mkataba na Yanga huku akiwa bado ana mkataba na Wekundu hao ambapo vijana Wamsimbazi wanahitaji kulipwa fidia kubwa kutokana na kitendo hicho.

Ofisa Habari wa TFF Alfred Lucas alisema suala kwa sasa lipo kwa msuluhishi ambaye ni Mjumbe wa FIFA Mzee Saidi El Mamry ambapo pande zote mbili zinatakiwa kufanya maridhiano ili kutoa maamuzi ambayo yatakuwa ya busara.

Lucas alisema endapo pande zote zitashindwa kufikia muafaka basi suala hilo litarudishwa kwenye Kamati hiyo na litamalizwa haraka kwa mujibu wa kanuni za TFF.

"Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji ilikaa juzi Jumamosi lakini upande wa Yanga uliomba shauri hilo lisogezwe mbele kwavile Wakili wao Mgongolwa alipatwa na msiba kwahiyo Alhamisi saa 11 jioni ndiyo hukumu itatolewa," alisema Lucas.

Post a Comment

 
Top