BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Kibaha
MKUFUNZI wa waamuzi wa CAF, Riziki Majala ameweka wazi kuwa mwamuzi wa kike Jonesia Rukyaa ataendelea kuwa mwamuzi bora kuchezesha mechi za Ligi Kuu Bara (VPL) tofauti na baadhi ya waamuzi wengine wa kiume ambao hawajafikia kiwango chake.

Jonesia ambaye ameteuliwa kwenda kuchezesha fainali za Kombe la Afrika kwa Wanawake zitakazoanza Novemba 19 nchini Cameroon anastahili kuchezesha ligi kuu kwani amekidhi viwango vyote vinavyotambulika na FIFA.

Katika mahojiano maalumu na BOIPLUS yaliyofanyika mjini Kibaha, Majala alisema kuwa mwanamama huyo aliweza kufuzu mitihani yote ya Fifa na ndio maana alipewa beji hiyo ya kimataifa.

Baadhi ya mitihani mikubwa ambayo mwamuzi anapaswa kufuzu ni sheria za soka, mtihani wa afya na utimamu wa mwili.


Riziki Majala

"Si kweli kuwa mwamuzi wa kike hapaswi kuchezesha mechi ya wanaume kama ilivyo kwa Jonesia, kuna mafunzo wanapewa ambayo akifuzu katika kiwango cha wanaume basi anachezesha tu pasipo shaka.

"Jonesia naweza kusema ni mwamuzi bora kuliko hata waamuzi wengine wa kiume kwani amekuwa akifanya mitihani mara nne kwa mwaka wakati wanaume wanafanya mara mbili, pia kila mwezi kuna mitihani ya Fifa anafanya ambayo ni ya kujitathimini hapo huwezi kusema hana vigezo," alisema Majala.

Majala alisema kuwa waamuzi wa kike ni lazima wapate mechi za kuchezesha mara kwa mara ili waweze kufikia ngazi ya kimataifa.

"Hata Jonesia mara ya kwanza walimdharau lakini alipochezesha vizuri mechi ya kwanza ndipo TFF walianza kumwamini, hivyo ili idadi ya waamuzi wa kike wenye beji ya Fifa iongezeke ni lazima wawape nafasi ya kuchezesha mechi nyingi," alisema na kuongeza.

"Jonesia sasa anakwenda kuchezesha michuano mikubwa hiyo ni hatua nzuri na ni sifa kwa Taifa letu, tuwape nafasi wanawake ya kuwaamini," alisema Majala.

Post a Comment

 
Top