BOIPLUS SPORTS BLOG


Sheila Ally, Dar
KIUNGO mkongwe wa Mbeya City, Ramadhan Chombo ' Redondo' amesema kuwa ubingwa wa msimu huu hauna mwenyewe kwani muda wowote matokeo yanabadilika ila wao wamejiweka katika tano bora za Ligi Kuu ya Vodacom.

Akizungumza na BOIPLUS, Redondo alisema kuwa ligi imekuwa ngumu, haitabiriki ingawa timu zenye kipato cha chini ndizo zitaathiriwa zaidi kwani muda mwingi wanautumia barabarani kusafiri kuwafuata wapinzani wao kuliko kujiandaa.

Alisema kuwa hiyo ndiyo changamoto pekee kubwa ambayo imeziathiri timu nyingine ukiachana na Simba, Yanga pamoja na Azam ambazo zina uwezo wa kusafiri kwa kutumia usafiri wa anga pale ambapo wanaona safari yao ni ndefu.

"Kila mtu anatamani kuwa juu ya mwenzake ila sisi tunataka kuwemo kwenye tano bora, timu nyingi zinaumizwa na ratiba jinsi ilivyokaa hasa sisi ambao timu zetu uwezo wa kifedha ni mdogo. Ila ikumbukwe kwamba hii ligi ni ngumu na haina mwenyewe ndio maana mnaona hata wale waliokuwa wanafanya vizuri nao wameteleza.

"Huo ndio ugumu wa ligi huwezi kumaliza safari pasipo kujikwaa na mwingine kunyanyuka hata sisi tunaitamani hiyo nafasi ya juu ingawa tumeweka malengo kwamba tupiganie kwanza tano bora," alisema Redondo.

Kiungo huyo wa zamani wa Simba, Azam na Taifa Stars, alisema anaamini benchi la ufundi litafanya mabadiliko kwenye kikosi chake ambayo yataisaidia timu mzunguko ujao wa ligi.

"Tulianza vizuri lakini pia hatujamaliza vibaya, kuna mapungufu kwenye timu ambayo benchi la ufundi naamini watayafanya ili mzunguko ujao timu iwe na upinzani mkubwa," alisema.

Post a Comment

 
Top