BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu

HATMA ya mfanyabiashara Mohamed Dewji 'MO' kutaka kununua hisa za klabu ya Simba kwa asilimia 51 sasa itajulikana Disemba 11 baada ya uongozi kuitisha Mkutano Mkuu wa dharura, mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ilikutana juzi Novemba 18 chini ya Rais, Evans Aveva na kupitisha kwa kauli moja mkutano huo wa mabadiliko ya katiba ambao utaruhusu MO kuwekeza Sh 20 bilioni kama alivyotamka hapo awali.

Kamati ya Utendaji ina mamlaka ya kuitisha mkutano huo kwa mujibu wa Katiba ya Simba Ibara ya 22 kifungu cha kwanza ambapo nyaraka za mkutano huo zitatolewa kwa wanachama wao kupitia matawi yote ya Simba kwa muongozo wa Ibara ya 22 kifungu cha nne cha Katiba yao.

Septemba, Baraza Michezo la Taifa (BMT) kupitia Katibu mkuu Mohamed Kiganja lilipiga marufuku kwa klabu za Simba na Yanga kufanya mabadiliko ya kiundeshaji hadi hapo zitakapofuata taratibu kwa mujibu wa Katiba zao ambapo sasa Wekundu hao wameanza kufuata maelekezo hayo.

Hata hivyo Kiganja, amesisitiza kuwa, Katiba ya Simba iliyopo na inayotambuliwa kwa msajili ni ile ya 2010 ambayo ina mapungufu mengi hivyo wanapaswa kuwa makini na ili mchakato huo ukamilike na kupitishwa ni lazima msajili wa vyama vya michezo aikubali na kugonga mhuri na si vinginevyo.

"Wafanye mkutano wao maana kila kitu kipo wazi, utaratibu unajulika na mabadiliko ya Katiba nayo si jambo la mara moja hivyo taratibu zifuate na mengine yatafuata," alisema Kiganja.

Post a Comment

 
Top