BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Shinyanga
BEKI wa Prisons, Salum Kimenya ameanza kufikiria kuachana na timu hiyo ili kwenda kupata changamoto mpya nje ya Jeshi la Magereza ambapo amedumu kwa zaidi ya miaka mitatu.

Kimenya ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa wakitajwa kila dirisha la usajili linapofunguliwa kusajiliwa na Wekundu wa Msimbazi, Simba lakini imekuwa ngumu kunasa saini yake kwani wanashindwa kufikia makubaliano ya kifedha hasa pesa ya usajili.

Kimenya amekuwa akitoa masharti magumu kwa mabosi wa Simba kwamba endapo wanamuhitaji basi wampe dau nono kwa wakati mmoja tofauti na pale vigogo hao wanapomuahidi kumpa kwa awamu.

Habari zaidi zinadai kuwa, Kimenya ambaye ni mwajiriwa wa Magereza sasa ameona ni muda muafaka wa kuachana na timu hiyo ingawa mkataba wake umebaki wa mwaka mmoja na huenda akafanya maamuzi hayo pale atakapopata sehemu sahihi ya kucheza huku ikitajwa kuwa wakati wa dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Novemba 15.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya Prisons kilisema kuwa Kimenya ambaye hivi karibuni ametoka masomoni alikopelekwa na jeshi hilo kilisema kuwa mawazo ya beki huyo kwasasa ni kuangalia mbele zaidi.

"Sheria zetu huwa hazitubani sana, kwani unapoamua kuacha kazi ndipo hapo mkataba wako unakuwa umemalizika ingawa tunakuwa na mikataba miwili ya ajira ya jeshi la Magereza na ile ya timu, hivyo ni rahisi tu kama ataamua kuondoka," kilisema chanzo hicho.

Alipoulizwa Kimenya alisema kuwa; "Bado nina mkataba na Prisons lakini nikipata sehemu nyingine ambapo patakuwa na masilahi naweza kuondoka, huwa sipendi kuondoka sehemu kwa ugomvi bali taratibu zikifuata na mimi nikaridhia hakutakuwa na tatizo lolote, ni kweli natamani sasa kupata changamoto mpya.

"Nina mkataba na Prisons ndiyo maana nasema ni mchezaji halali wa timu hiyo, ila muda ukifika naweza kuondoka kwa kufuata taratibu zote," alisema Kimenya.

Post a Comment

 
Top