BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Malimi Busungu yupo kwenye mchakato wa kuhakikisha makali yake yanarudi na ameweka wazi kuwa makali hayo yatarudi pale tu atakapopata timu ya Ligi Kuu na tayari baadhi ya timu zimeanza  kutuma maombi ikiwemo Stand United na Majimaji.

Busungu ambaye aling'ara wakati yupo na Mgambo JKT alianza kufukuziwa na Simba lakini Yanga ndiyo waliwazidi ujanja watani wao na kumpa mkataba wa miaka miwili ambao unamalizika mwishoni mwa msimu huu.

Stand United wamekiri kuwepo na mipango hiyo lakini hatima ya mambo yote ya usajili itajulikana kesho Jumamosi wakati kocha Athuman Bilali akikabidhi ripoti ambayo itajadiliwa kesho hiyo hiyo.

Katibu Mkuu wa Stand United, Kennedy Nyangi aliiambia BOIPLUS kuwa' "Kuna mambo mawili, usajili na kocha. Bilali ni kocha mzuri ila amekuwa mpole sana kwa wachezaji kiasi kwamba wanamuonea na kufanya mambo ya utovu wa nidhamu. Hivyo hili tunaliangalia na kama tungepata mdhamini tungekuwa tumepata kocha mwingine ambaye angesaidiana na Bilali.

"Kuhusu usajili tutaangalia mapendekezo ya mwalimu yakoje ila Busungu ni mchezaji  mzuri lakini hatuwezi kusema moja kwa moja kuwa tunamchukua ama lah," alisema Nyangi.

Kwa upande wa Busungu alifafanua kwamba, "Nina mkataba na Yanga ambao unamalizika msimu huu, sio Stand tu waliotuma maombi bali ni timu nyingi ila natakiwa kutulia kuangalia wapi patanifaa na si kwa kuvunja mkataba na Yanga.

"Barua zimekuja nyingine za kuniomba kwa mkopo na ninadhani nitaenda kwa mkopo kwani ninachokihitaji ni kupata nafasi ya kucheza, naumia kuona nakosa nafasi wakati bado najiamini kuwa naweza kucheza, nimetambua wapi nilijikwaa pia," alisema Busungu na kuongeza.

"Kama kutakuwepo na haja ya kuvunja mkataba na Yanga hayo ni makubaliano mengine ila sijafikiria kuomba kuvunja mkataba kwasasa," alisema Busungu.

Post a Comment

 
Top