BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 'Serengeti Boys' Bakari Shime amechukua mikoba ya Malale Hamsini kuwanoa Maafande wa JKT Ruvu kuanzia mzunguko wa pili wa ligi utakaoanza Disemba 17.

Maafande hao wamefanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi ambapo Shime atasaidiwa na Koplo Alex Mwamgaya kocha wa makipa ni Sajini Abdallah huku Mkurugenzi wa Ufundi akiendelea kuwa Abdallah Kibadeni. 

Ruvu wameingia kambini Novemba 25 kujiandaa na mikikimikiki ya duru la pili la ligi kwenye Uwanja wa JKT Mbweni chini ya kocha huyo wa zamani wa Mgambo JKT ya jijini Tanga ambayo sasa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Ofisa Habari wa JKT RUVU, Constantine Masanja alisema uongozi wa timu hiyo umeamua kufanya marekebisho kwenye benchi la ufundi ili kuhakikisha wanafanya vizuri baada ya kuvurunda mzunguko wa kwanza ambapo wanashika nafasi ya 14 wakiwa na pointi 13.

"Uongozi umefanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi sasa kocha mkuu ni Shime akisaidiwa na Mwamgaya pamoja na Sajini Abdallah," alisema Masanja.

Masanja alisema kuhusu usajili uongozi umemuachia kocha Shime kuamua kupunguza au kuongeza wachezaji kabla ya kufungwa dirisha la usajili huo, Disemba 15.

Post a Comment

 
Top