BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
LICHA ya kuonekana kufanya makosa ya wazi yaliyopelekea timu ya Simba kupoteza mechi zake mbili za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi mlinda mlango Vicent Agban amekingiwa kifua na kocha wake Adam Meja.

Agban amedaka mechi zote 15 za mzunguko wa kwanza lakini katika mechi kadhaa za mwisho alionekana akifanya makosa mengi yaliyoigharimu timu hiyo mpaka wapinzani wao Yanga kupunguza idadi ya pointi kutoka nane hadi mbili kwa sasa.

Meja ameiambia BOIPLUS kuwa kipa huyo yuko makini langoni pia anafanya vizuri mazoezini ndiyo maana amepata nafasi ya kucheza mechi nyingi na makosa anayofanya ni ya kawaida ambayo kipa yoyote anaweza kufanya.

"Agban sio kipa mbaya kama watu wanavyodhani ila kinachotokea ni kawaida kwenye soka watu wanaomshutumu leo wakumbuke ndiyo wao waliokuwa wanamsifu katika mechi zetu za awali alipokuwa hajafungwa, wakati mwingine binadamu hawana wema," alisema Kocha huyo.


Meja alisema pia alielezea juu ya uwezo wake wa kufundisha akijinasibu kuwa amesomea fani hiyo na sio kama watu wanavyosema kuwa yupo Simba kiujanja ujanja bali weledi ndiyo unaomuweka mpaka Uongozi utakapo amua vinginevyo.

"Fani hii nimesomea nilianza kozi ya awali ya ukocha iliyotolewa na Shirikisho la mpira wa miguu (TFF) kabla ya kuchukua level I ambayo Tanzania ilikuwa ni nchi ya tatu barani Afrika kupata kozi hiyo ambayo makocha wengi nchini wamepata," alisema Meja.

Meja anayetajwa kuondolewa Msimbazi aliwahi kuzidakia timu za Ashanti United, Vijana Ilala pamoja na JKU ya Zanzibar.

Post a Comment

 
Top