BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
Makamu mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga kushoto akimkabidhi jezi kocha mkuu mpya George Lwandamina

MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Clement Sanga amemtambulisha kocha mkuu wa timu hiyo Mzambia George Lwandamina pamoja Mkurugenzi wa ufundi Hans Pluijm mbele ya Waandishi wa Habari klabuni hapo mapema asubuhi ya leo huku mzambia huyo akifunguka juu ya kikosi atakachoingia nacho vitani.

Lwandamina anachukua mikoba ya Mholanzi Hans aliyebadilishiwa majukumu na kuwa mkurugenzi wa ufundi ili kumsaidia Mzambia huyo katika masuala mbali mbali ya maendeleo ya klabu hiyo.

Sanga alisema kuwa baada ya tetesi za muda mrefu kuhusu ujio wa kocha huyo sasa ni rasmi baada ya Lwandamina kusaini mkataba wa miaka miwili na vijana hao wa Jangwani ambapo mzunguko wa pili ataongoza jeshi hilo la kijani na njano kutetea Ubingwa wa ligi.

Lwandamina akisalimiana na Mkurugenzi mpya wa ufundi Hans Pluijm

"Uongozi wa Yanga unayo furaha kuwatambulisha kocha mkuu (Lwandamina) na mkurugenzi wa ufundi (Hans) ambao tunaamini kwa pamoja wataweza kuipa mafanikio zaidi timu yetu kutoka hapa ilipo na kusonga mbele zaidi" alisema Sanga.

Kwa upande wake Lwandamina alisema "ni changamoto mpya kwangu najua Yanga ni klabu kubwa nitahakikisha natumia kila kinachowezekana kuhakikisha tunafanya vizuri kuanzia kwenye ligi ya nyumbani hadi klabu Bingwa Afrika.

"Nasikia tetesi kuhusu wachezaji wapya kutoka Zesco kusajiliwa Yanga mimi kama kocha mkuu sijui chochote labda michakato hiyo inafanyika bila mimi kushirikishwa kikosi kilichopo ndicho nitaendelea nacho" alisema Lwandamina.

Nae Mkurugenzi mpya wa ufundi wa klabu hiyo alisema yeye hana shida na kubadilishiwa majukumu kikubwa ataendelea kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba wake.

Post a Comment

 
Top