BOIPLUS SPORTS BLOG

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Shirikisho la Mpira wa miguu Brazil (CBF), kufuatia vifo vya wachezaji wa timu ya soka ya Chapecoense Real ya Brazil kwa ajali ya ndege.

Katika salamu za rambirambi kwa Rais wa CBF, Lucca Victorelli, Malinzi amesema ajali hiyo iliyoua watu wengi ni tukio la kusikitisha kwenye familia ya soka duniani na limetokea katika kipindi kigumu.

Malinzi ambaye alituma salamu hizo pia kwa mashabiki wa Chapecoense na Jumuiya ya soka na wanafamilia wengine wa nchini Brazil, alisema "Mawazo yetu yapo kwa wahanga wa ajali hiyo, familia na jamaa zao,".

Ndege hiyo iliyokuwa ikisafiri juzi Jumatatu kutoka Brazil kupitia Bolivia kwenda Colombia ilibeba abiria 81 wakiwamo wafanyakazi na wachezaji wa Chapecoense ya Brazil kabla ya kuanguka kwenye milima ya Colombia.

Wachezaji hao wa Chapecoense  waliokuwa wakisafiri kwenda kucheza mechi ya fainali ya michuano ya ubingwa wa Kombe la Amerika ya Kusini (Copa Sud Americana), walikuwa ni miongoni mwa abiria 81.

Michuano hiyo ni ya pili kwa ukubwa katika Bara la Amerika ya Kusini, iliyotarajiwa kuchezwa leo Jumatano Novemba 30, ambako Chapecoense ingecheza dhidi ya Atletico Nacional ya Colombia.

Rubani wa ndege hiyo alitoa taarifa ya hali ya hatari iliyosababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa umeme, kabla haijaanguka muda mfupi baadaye karibu na Mji wa Medelin.

Taarifa za vifo hivyo, zimethibitishwa na Mkuu wa Mamlaka ya Anga ya Brazil, Alfredo Bocanegra aliyesema walionusurika ni watu watano wakiwamo wachezaji watatu wa Chapecoense na wafanyakazi wawili wa ndege hiyo.

Wachezaji walionusurika wanatajwa kuwa ni Alan Ruschel, golikipa Danilo na Jackson Follmann na kwamba walipatiwa huduma ya kwanza katika hospitali iliyoko katika mji wa Le Ceja nchini Colombia.

Post a Comment

 
Top