BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
Salum Kimenya kushoto akitafuta mbinu za kumzuia Mohamed Hussein 'Zimbwe' wa Simba

MAMA mzazi wa beki Salum Kimenya, amemruhusu mwanaye kujiunga na Simba endapo watafikia makubaliano ya kusaini mkataba wa miaka miwili lakini kwa sharti moja tu la kumpanga kikosini na si vinginevyo.

Kimenya anayekipiga katika timu ya Prisons yupo kwenye mazungumzo na Simba ambao wamekuwa wakimuwinda kila mara lakini wanashindwa kumnasa kutokana na dau analolitaka.

Hii ni mara ya tatu Simba kufanya mazungumzo na Kimenya ambapo safari hii viongozi wa Simba wamekutana na kisiki chenyewe baada ya Kimenya kuwataka kumalizana na mama yake anayefahamika kwa jina la Asia Salum ambaye ndiye mshauri wake mkuu.


Kimenya vs Hamis Kiiza


Akizungumza na BOIPLUS kutoka Urambo, Tabora, mama huyo alisema kuwa hana tatizo la mwanaye kucheza Simba ila kuna mambo ambayo Simba wanapaswa kuzingatia ikiwemo kumpanga kikosini pamoja na pesa ya usajili.

Imeelezwa kuwa Simba wapo tayari kumpa Kimenya Sh 25 milioni kati ya Sh 40 milioni ambayo beki huyo ameitaka baada ya kushuka kutoka Sh 50 milioni.

"Ni kweli Simba nimezungumza nao lakini  hatujafikia makubaliano hasa kwenye pesa wanayotaka kumpa, huyu ni mtumishi na anapoondoka anaacha ajira hivyo hiyo pesa ni ndogo maana anatakiwa kuilipa hata timu yake kwani anavunja mkataba.


Kimenya vs Azam FC


"Kimenya ni mwanangu na hiyo kazi ameipata baada ya mimi kumhangaikia kwa kumsomesha hivyo halitakuwa jambo la busara kuacha kazi kwa masilani madogo, simkatazi kwenda Simba ila masilahi yanatakiwa kuangaliwa pia," alisema na kuongeza.

"Pia nimewaambia mwanangu akienda pale acheze sio kuwa wakimsajili basi asipewe nafasi maana najuwa uwezo wake na hilo wamenihakikishia kuwa atacheza. Sina hofu na mwanangu juu ya utendaji kazi wake, hivyo nawasubiri wao maana walisema watanipigia tena simu," alisema mama Kimenya.

Kwa upande wa Kimenya alisema kuwa, "Mama yangu ndiye kila kitu katika maisha yangu, ndio maana hata hili suala nashauriana naye atakavyoamua nitafuata kwani naamini hawezi kuamua vibaya juu ya maisha yangu,".

Kuona story zote ndani ya BOIPLUS bofya HAPA

Post a Comment

 
Top