BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KLABU ya Simba imesikitishwa na kauli ya Katibu mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja kuwa mkutano wao mkuu wa dharura wa mabadiliko ya katiba uliopangwa kufanyika Disemba 11 maamuzi yake hayatakuwa na mashiko mpaka yapitishwe na Baraza hilo.

Jana Kiganja aliwaambia Waandishi wa Habari kuwa mkutano huo ni ruksa kufanyika kama utafuata sheria na taratibu zote kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo lakini mwisho wa siku maamuzi yatakayopitishwa lazima yapitie kwa msajili na baadae kufika kwa baraza hilo.

Ofisa Habari wa klabu ya Simba Haji Manara alisema mkutano huo umefuata taratibu zote na maamuzi yake hayatapitia sehemu nyingine yoyote na wameshangazwa na kauli ya Kiganja kuwa hata wakijadiliana lakini maamuzi yatoke BMT.


Manara alisema wanaiheshimu BMT kwakua ipo kwa mujibu wa sheria za nchi lakini haina mamlaka ya kuingilia mambo ndani ya klabu hiyo kwavile katiba inakataza na mabadiliko ya kiundeshwaji hayaepukiki kwa namna yoyote.

"Kiganja anasema mkutano ufuate utaratibu zote kwa mujibu wa katiba yetu lakini maamuzi lazima yafike kwao wayapitie wao wakati Waziri wa Habari Nape Nnauye alisema haina shida kama mkutano upo kwa mujibu wa katiba ya Simba," alisema Manara.

Manara alienda mbali zaidi na kusema kuwa BMT inaonekana wakati wa matatizo tu kwenye maendeleo haionekani kitu ambacho kinatia walakini.

"Mbona hawakutusaidia kuzitoa nyasi zetu bandia bandarini na vipi kuhusu mishahara ya wachezaji mbona hawatusaidii kulipa lakini kwenye Mkutano wanasema watatoa maamuzi hilo suala halipo" alisema Manara.

Post a Comment

 
Top