BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
UONGOZI wa Ruvu Shooting umeiandikia barua Bodi ya Ligi/TFF kuiomba mchezo wao na Yanga uliopangwa kuchezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Uhuru usogezwe mbele hadi  Taifa Stars itakaporejea kutoka Zimbambwe itakakocheza mechi ya kirafiki ya Fifa.

Taarifa iliyotolewa na Ruvu Shooting na Msemaji wao Masau Bwire imeeleza kuwa maombi hayo ni kutokana na hali ya usafiri na uchovu kwa wachezaji wao wanaotarajia kuwasili kesho Jumanne saa 1 asubuhi wakitokea Bukoba ikiwa ni siku moja kabla ya kuvaana na Yanga.

Masau alisema kuwa; "kutoka Bukoba hadi Kibaha ni umbali wa Kilomota 1,450 kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani, mwendo wa gari unatakiwa uwe KM 80 kwa saa, kwa maeneo yasiyo makazi ya watu na KM 50 kwa saa, kwa maeneo ya makazi ya watu. 

"Kwa wastani gari lililowabeba wachezaji wetu ambalo liko njiani mpaka sasa, linakwenda mwendo wa KM 65 kwa saa.
Kwa mwendo huo, yatahitajika masaa 22 dk 18 ili kukamilisha safari hiyo ndefu ya kutoka Bukoba hadi Kibaha, Mlandizi. 

Kwakuwa safari ilianza saa 3 asubuhi ya leo November 7, kama safari itakwenda salama, tunatarajia kesho saa 1.42 asubuhi timu kuwasiri Mlandizi," alisema Masau na kuongeza.

"Katika hali hiyo, safari ndefu yenye kuchosha, mchezaji bila kupumzika afikie mchezo mwingine, itakuwa ni mchezo wa upande mmoja, usio na ushindani ambao utaipa timu pinzani ya Yanga ushindi kwani, itakuwa inacheza na timu chovu kwa uchovu wa wachezaji kwa safari ndefu na kukosa muda wa kupumzika japo kwa siku moja," alisema.

Ruvu Shooting imeomba Bodi ya Ligi/TFF kuona kama kuna uwezekano wa kuusogeza mbele mchezo huo basi uchezwe Novemba 10 ili kuwapa wachezaji wao muda wa kupumzika na kuupa mchezo ushindani.

"Bodi ya Ligi/TFF waliliona hilo wakafanya mabadiliko ya mchezo huo kutoka Novemba 10 hadi 11. Lakini siku chache baadaye walifanya mabadiliko mengine kuhusu siku ya mchezo huo, kutoka Novemba 11 hadi 10 na baadaye wamefanya mabadiliko mengine ya siku ya mchezo huo huo kuwa Novemba 9 jambo ambalo litatuumiza tunaomba waliangalie upya," alisema Masau.

Post a Comment

 
Top