BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom, wameshindwa kupunguza tofauti ya pointi kati yake na vinara Simba baada ya kukubali kichapo cha bao 2-1 dhidi ya Mbeya City mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya huku ushindi huo ukiwa ni wao kwanza dhidi ya Yanga tangu kuanzishwa kwake.

Hassan Mwasapili aliipatia City bao la kwanza dakika ya sita baada ya kupiga mpira wa adhabu ulioingia moja kwa moja wavuni upande wa kushoto na kumwacha mlinda mlango wa Yanga Deogratius Munishi Dida' akiwa hana la kufanya.

Baada ya bao hilo City waliendelea kuonyesha kandanda safi ambalo liliwavuruga watoto wa Jangwani ambao sasa watakuwa wanaachwa pointi nane na vinara Simba walioifunga Stand United bao 1-0 leo katika dimba la CCM Kambarage.

Kenny Ally alifunga bao la pili dakika ya 36 kwa shuti kali la chini chini baada ya kutengewa mpira wa adhabu ambapo wachezaji wa Yanga walishindwa kuuzuia. Bao hilo lilimuweka kwenye wakati mgumu mwamuzi Rajabu Mrope kutoka Ruvuma baada ya kukubali awali na kulikataa tena kabla ya kukubali kwa mara nyingine.

Bao pekee la Yanga lilifungwa na Donald  Ngoma dakika 45 kwa kichwa baada ya kupokea pasi kutoka kwa Simon Msuva wakati walinzi wa City wakiachwa solemba na mtego wao wa kuotea.

Yanga wameendelea kubaki nafasi ya pili wakiwa na pointi 27 huku City wakifikisha pointi 19 ambazo zitawaweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi kutegemea matokeo mengine ya mechi za leo.

Post a Comment

 
Top