BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
SIMBA ilimsajili beki mkongwe kutoka Caps United ya Zimbabwe, Method Mwanjali ambaye ana msaada mkubwa kwenye kikosi hicho lakini Mbeya City nao wameonyesha nia ya kwenda nchini humo kumsaka straika Leonard Tsipa ambaye anacheza timu hiyo.

Kocha wa Mbeya City, Kinnah Phiri, amesema kuwa hamfahamu mchezaji huyo ila ameletewa na rafiki yake ambaye ni wakala kwamba amwangilie na kujiridhisha lakini kiungo wa zamani wa Simba, Justice Majabvi amesema kama City wataamua kumsajili straika huyo basi watakuwa wamelamba dume huku Mrundi Hemed Murutabosa kibarua chake huenda kikaota nyasi.

Phiri tayari amefanya mazungumzo na wachezaji wanne mpaka sasa wanaocheza Ligi Kuu ya Vodacom ambao ni Tito Okello na Hood Mayanja wote ni washambuliaji wanaoichezea African Lyon ingawa sasa mikataba yao imemalizika pamoja na kipa Abraham Chove na beki wa kushoto, Paul Ngalema ambao wote wanacheza Ndanda FC.

"Okello na Mayanja nimekutana nao jana Jumanne pale Uwanja wa Ndege wakati naelekea Mbeya, tumezungumza na sasa kazi ya mwisho nimewaachia viongozi ikiwemo Chove na Ngalema. Huyo Mzimbabwe nasubiri kumuona ingawa nahitaji kuwa na washambuliaji wazuri na wazoefu tofauti na waliopo sasa ambao si wazoefu na wanashindwa kufunga wapatapo nafasi," alisema Phiri.


Akimzungumzia straika huyo, Majabvi alisema kuwa; "Namfahamu na ni mchezaji mzuri wakimpata atawasaidia, ana uzoefu na anaweza kufunga,".

Tsipa aliyezaliwa Januari, 25, 1982 amewahi pia kuzichezea timu za FK Javor, Dynamos na Gunners Harare.

Kwa upande wa Chove, alikiri kuwepo kwa mazungumzo kati yake na Mbeya City; "Mimi sina tatizo, kocha Phiri ananifahamu tangu nilipokwenda kucheza soka Malawi miaka ya nyuma, hivyo nawasubiri wao kwani nimemuweka wazi kuwa nilisaini mkataba wa mwaka mmoja, hivyo kuna taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa, tangu msimu uliopita wananihitaji,".

Kwasasa Mbeya City wamekwenda mapumziko mafupi ambayo yatamalizika Novemba 25 huku usajili wa dirisha dogo ukitarajiwa kufunguliwa rasmi wiki ijayo, Novemba 15.

Post a Comment

 
Top