BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
BEKI wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein 'Zimbwe jr' amebakiza mkataba wa miezi sita tu na sasa anaruhusiwa kufanya mazungumzo na timu yoyote na tayari milango imefunguliwa kwake kwani hadi sasa timu yake ipo kimya.

Beki huyo aliyesajiliwa Simba akitokea Kagera Sugar miaka mitatu iliyopita ametajwa pia kuwaniwa na Yanga ingawa habari hizo hazijawekwa wazi na Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara ambapo ofa ya awali waliyoiweka mezani kwa Simba ni Sh 40 milioni ambayo ndiyo ilikuwa ikijadiliwa.

Meneja wa mchezaji huyo, Herry Mzozo aliiambia BOIPLUS kuwa mpaka sasa hajapokea ofa kutoka timu yoyote na hata Simba hajamalizana nao japokuwa walifanya mazungumzo kipindi cha nyuma ingawa uongozi wa Simba uliwahi kunukuliwa ukisema hawana wasiwasi juu ya kumwongeza mkataba mpya Zimbwe.Mzozo alisema kuwa soka ndiyo ajira ya mteja wake hivyo kwa timu yoyote itakayoonyesha nia ya kumsajili basi yupo tayari kufanya nayo mazungumzo na atamruhusu Zimbwe kwenda kuichezea timu itakayotoa donge nono.

"Simba tulifanya nao mazungumzo tu ila hadi sasa wapo kimya, kiukweli sijapokea ofa kutoka timu yoyote kwa sasa ikimuhitaji Zimbwe na kama zitakuja sitosita kuzungumza nazo na kufikia makubaliano kama tutaridhika.

"Simba ni timu ambayo niliipa kipaumbele ila wapo kimya, hivyo tunaendelea kusubiri ila hatutaacha ofa zitakazokuja mbele yetu, mashabiki na wanachama wa Simba wanathamini mchango wa Zimbwe ndiyo maana nafasi ya kwanza ni kwao, hivyo ngoja tuone inakuwaje, hao Yanga kwasasa nimesikia kwenye vyombo vya habari kama wanamuhitaji basi watakuja," alisema Mzozo.

Mzozo alifafanua zaidi kuwa timu itakayomtaka ifuate taratibu na kanuni za usajili, "Kwanza atakayekuja ajue kufuata taratibu za mkataba kwani sisi tukipata ofa tutaipeleka Simba kuwaambia mteja wangu anatakiwa na timu fulani hivyo taratibu za kuvunja mkataba kwa miezi itakayobaki zitafuatwa,".

Post a Comment

 
Top