BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
BEKI wa zamani wa Azam, Said Morad ameshindwa kuvumilia na kutoa la moyoni kuhusu mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta kuwa anapaswa kupiga hatua na kucheza ligi nyingine za Ulaya kama Ufaransa ama 
Uingereza.

Kauli hiyo aliitoa katika mahojiano maalumu na BOIPLUS yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, kwamba siku zote hupenda kuona wachezaji wa kitanzania 
waliobahatika kucheza soka la kulipwa wakifanikiwa zaidi ya walipofikia.

Morad alisema kuwa mara kadhaa alipokutana na Samatta pamoja na mwenzake Thomas Ulimwengu wakiwa TP Mazembe jambo kubwa aliwaambia kila mmoja apambane katika kupachika mabao hasa pale anapopata nafasi ya kucheza akiwa Taifa Stars ama kwenye klabu yake.

"Nilikuwa nakutana nao kwenye timu ya Taifa  niliwaambia kabisa kuwa wao ndiyo nyota wetu wanapaswa kupambana kila mechi kufunga, kama sio Samatta basi Ulimwengu na ikiwezekana wote wafunge. Hatua ya Samatta kwasasa ni kubwa na hatakiwi kuishia hapo asonge mbele zaidi.

"Wapo wachezaji wengi wanacheza nje kama Mrisho Ngassa akina Humud na 
wengine wajitahidi kupambana zaidi kufikia mafanikio waliyojiwekea maana 
wenzetu wamepata bahati ya kuonja soka la kulipwa, hawapaswi kurudi nyuma," alisema Morad.

Beki huyo kwasasa amejiwekea utaratibu wa mazoezi binafsi akisubiri kusajiliwa na timu yoyote kwamba Jumatatu na Jumanne huwa anafanya mazoezi ya kukimbia barabarani, Jumatano hadi Ijumaa anakuwa kwenye mazoezi ya uwanjani na Jumamosi huwa anacheza mechi mtaani kwao.

"Mchezaji hata kama huna timu unapaswa kuwa fiti muda wote ndiyo maana nafanya mazoezi kila siku na baada ya hapo huwa napumzika, nipo kwenye mipango pia ya kununua vifaa kwa ajili ya gym nyumbani kwangu," alisema Morad.

Post a Comment

 
Top