BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
Said Morad kushoto akichuana na Donald Ngoma

BEKI wa zamani wa Azam FC, Said Morad ameweka wazi mastraika waliokuwa wakimsumbua hasa timu yake ilipokutana na wapinzani mbalimbali kuwa baadhi yao ni Donald Ngoma, Atupele Green, Fully Maganga akiwemo Emmanuel Okwi.

Kwa upande wa Amissi Tambwe amemuelezea kuwa Mrundi huyo si straika msumbufu kwani yeye hutulia katika eneo moja tu la ufungaji huku akimtaja pia John Bocco kuwa hana tofauti na akina Ngoma.

Akizungumza na BOIPLUS, Morad alisema kuwa hao ni baadhi tu ila anaamini akipata timu ya Ligi Kuu Bara basi Bocco atamsumbua sana kwani uwezo wake sawa na Ngoma ama Maganga au Atupele.

Morad akiwa mazoezini na John Bocco

"Najua ipo siku nikiwa na timu nyingine nitakutana na Bocco, Ngoma na hao wengine, kiukweli hawa washambuliaji ni wasumbufu sana kwani wanajuwa kuruka juu, wanakwenda chini na hata kupambana pia tofuati na Tambwe ambaye hutulia sehemu moja," alisema Morad na kuongeza.

"Wachezaji wapo wengi wazuri ila kila mchezaji ana ubora wake kutokana na jinsi anavyopambana ndio maana Tambwe hawezi kuwa kama Ngoma ama Bocco, Tambwe ana kazi ya kufunga tu," alisema Morad.

Morad pia aliwataka wachezaji kujitunza ili wacheze kwa kipindi kirefu soka lao na kwamba wapatapo mafanikio wakumbuke kuwekeza kwenye mambo ya maana.

"Kila kitu ukitaka kufanya unaweza pale unaposhika pesa, ila hawa wadogo zetu wakumbuke kuwekeza hata kwa kujenga nyumba kwani mpira una muda wake," alisema Morad.

Post a Comment

 
Top