BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
KAGERA Sugar inaweza kumkosa kipa wao Hussein Sharrif  'Casillas' baada ya timu ya DC Motema Pembe ya DR Congo kuonyesha nia ya kuhitaji huduma yake mwezi ujao, Desemba.

Casillas kwasasa amesimamishwa kwa tuhuma za kuhujumu timu hiyo ilipofungwa bao 6-2 na Yanga kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Casillas aliwahi kwenda kufanya majaribio na timu hiyo ambapo walimuahidi kumuita baada ya kufuatilia maendeleo yake zaidi kwenye mechi za VPL na sasa imeelezwa kuwa kipa huyo ameitwa kwenda kufanya mazungumzo ya mwisho.

Meneja wa mchezaji huyo, Shomari Ndizi, ameiambia BOIPLUS kuwa kama mambo yake na Kagera Sugar yatashindwa kumalizika basi atalazimika kuondoka ili akacheze huko na kwamba atapata changamoto mpya.

"Bado hatujaambiwa lolote kuhusu uchunguzi wao umefikia wapi, hivyo tunaendelea kuwasubiri watasemaje, ila Motema Pembe wamewasiliana na  sisi wakimuhitaji Casillas kwenda kufanya nao kazi, endapo Kagera wataamua kumrejesha kikosini basi hao watapaswa kufuata taratibu za usajili.

"Kama Kagera watasema hawamuhitaji basi itabidi aangalie maisha mengine ya kucheza soka nje nchi, maana maisha ya Casillas yanaendeshwa na mpira akikaa bila kucheza itamuathiri," alisema Ndizi.

Casillas alisajiliwa na Kagera Sugar akitokea Mtibwa Sugar ambako pia alikuwa hapati nafasi ya kusimama langoni mara kwa mara kutokana na upinzani mkubwa alioupata toka kwa Said Mohamed.

Post a Comment

 
Top