BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
WINGA wa timu ya Yanga Simon Msuva amekiri kuwa haikuwa kazi rahisi kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi wa ligi wakiwa nafasi ya pili kwa tofauti ya alama mbili nyuma ya Simba kutokana na ligi ilivyokuwa ngumu na ubora wa wapinzani wao.

Msuva alisema mzunguko huo ulikuwa na changamoto kubwa kwao kwani wapinzani wao walikuwa bora huku wakiwakamia sana wanapokutana ila wanamshukuru Mungu kwa kupunguza idadi ya pointi kutoka nane hadi kufikia mbili nyuma ya watani wao Simba.

Msuva ambaye amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi kwa mwezi Oktoba alisema mwanzoni mwa mzunguko walikuwa wakicheza kwa presha baada ya kushindwa kupata matokeo mazuri huku wapinzani wao wakifanya vizuri lakini walituliza akili na kucheza kwa malengo hadi kufikia kubakisha pointi mbili nyuma ya Simba.

"Ligi ilikuwa ngumu tumepambana sana hadi kufikia hapa, wenzetu walituacha pointi nyingi sisi hatukakata tamaa mpaka tumemaliza mzunguko tukiwa nafasi ya pili," alisema Msuva.

Katika ushindi wa jana dhidi ya Ruvu winga huyo alifunga bao la kwanza na kufikisha idadi ya mabao saba sambamba na mchezaji mwenzake Amissi Tambwe mabao mawili nyuma ya Shiza Kichuya wa Simba aliyetupia tisa.

Msuva ni miongoni mwa wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' walioondoka hii leo kuelekea nchini Zimbabwe kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa Kimataifa unaotambuliwa na Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA utakaochezwa keshokutwa Jumapili.

mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Vodacom umemalizika jana huku Wekundu wa Msimbazi Simba wakiwa vinara baada ya kujikusanyia alama 35 wakifuatiwa kwa karibu na Yanga wenye pointi 33 Azam wao wana pointi 25 nafasi ya tatu Toto African wao wanaburuza mkia wakiwa na alama 12.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF Alfred Lucas mzunguko wa pili utaanza kutimua vumbi Disemba 17.

Post a Comment

 
Top