BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
UONGOZI wa Simba leo mchana umekutana na beki wao Mohamed Hussein 'Tshabalala' kumalizia mazungumzo ya mkataba mpya wa miaka miwili  ambapo wamekubaliana kuwa  utasainiwa mara tu Simba watakapomuingizia fedha ya usajili kwenye akaunti yake ya benki.

Mazungumzo na makubaliano hayo yamefanyika ofisini kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe zilizopo Tangi Bovu, Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.Meneja wa mchezaji huyo, Herry Mzozo ameiambia BOIPLUS kuwa wamefikia makubaliano ya kumpa mkataba huo kwa kukubali ofa ya Sh 40 milioni baada ya kujadili kwa kina kwani kulikuwepo na mapendekezo ya ofa mpya.

Mzozo alisema kuwa mteja wake anaweza kusaini mkataba rasmi ndani ya siku hizi mbili hivyo mashabiki na wapenzi wa Simba wawe na uhakika wa kubaki na beki huyo.

"Kila kitu kimekwenda vizuri ila tumewaambia waingize kwanza pesa ndipo tusainishane mkataba hivyo wamesema watakamilisha taratibu za kibenki ndani ya siku mbili hizi, hivyo suala la Tshabalala sasa limekwisha," alisema Mzozo.Mzozo alisema kuwa tangu mwanzo waliipa Simba kipaumbele kutokana na jinsi walivyoishi naye kwa kumthamini huku akiweka wazi kwamba habari za beki huyo kutua Yanga hazikuwa na ukweli wowote kwani mabingwa hao watetezi wa ligi kuu hawakuwahi kufanya nao mazungumzo.

Kwa upande wa Azam alisema kuwa nao hawakuonyesha nia ila hata kama wangeonyesha nia bado nafasi ingekuwa kwa Simba kwani Tshabalala aliwahi kucheza Azam ila hawakuonyesha kumthamini hadi walipomuacha.

Post a Comment

 
Top