BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amewataka wadau waachane na dhana ya kila mgogoro unaotokea kwenye sekta ya michezo kuupeleka kwenye Mahakama za kiraia.

Kauli hiyo inakuja muda mchache  baada ya baadhi ya watu kwenda mahakamani kupinga Uchaguzi wa Chama cha Riadha Tanzania (RT) ambao uliopangwa ufanyike baadaye mwezi huu.

Nape aliwaambia Waandishi wa Habari kuwa imeanza kuwa ni utamaduni kwa kila anayedai haki yake au kutokuridhishwa na mambo yanayoendelea hasa yanayohusu masuala ya Uchaguzi kukimbilia mahakamani licha ya vyombo vinavyohusika kutatua migogoro hiyo kuwepo.

"Wizara ya Habari ipo, Baraza la Michezo lipo sasa kuna haja gani kukimbilia mahakamani kutafuta haki wakati wanaweza kuipata kupitia vyombo hivi,nashauri kila kitu kifuate utaratibu hakutakuwa na haja ya kukimbilia huko," alisema Nape.

Nape alisema kuwa kunapotokea mgogoro wowote kwenye chama chochote cha michezo wahusika wanapaswa kuchukua hatua za haraka kuutatua ili kuepuka watu kwenda mahakamani kudai haki.

Mwezi uliopita wanachama wawili wa Klabu ya Yanga, Frank Chacha na Juma Mangoma walienda mahakamani kupinga Mkutano Mkuu wa dharura uliopangwa kufanyika Oktoba 23 ambao miongoni mwa ajenda zilizokuwepo ni suala la kukodishwa kwa nembo ya timu hiyo kinyume na Katiba ya Mabingwa hao wa kihistoria nchini.

Post a Comment

 
Top