BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally
KLABU ya Mbeya City FC imezidi kuneemeka baada ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili na Kampuni ya Cocacola Kwanza, mkataba huo umesainiwa leo jijini Mbeya.

Huu ni mkataba wa pili kwa klabu hiyo baada ya awali kusaini mkataba na Kampuni ya Binslum iliyotoa Sh 300 milioni kwa miaka miwili, City ina mkataba mwingine na Benki ya Posta ambao si wa kifedha bali ni kwa ajili ya kuhamasisha mashabiki na wanachama.

Hafla hiyo ilifanyika kwenye Uwanja wa Sokoine ambapo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya akiwemo Mkurugenzi wa Jiji Zacharia Nachoha, Mstahiki Meya, David Mwashilindi pamoja na viongozi wa klabu hiyo.

Katibu mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe aliiambia BOIPLUS kuwa "Thamani ya mkataba inabaki kuwa siri ya pande mbili, klabu na kampuni ya Coca Cola, tunashukuru wamekubali kutuongeza mkataba mpya baada ya ule wa awali kumalizika Septemba ambao pia ulikuwa wa miaka miwili,".

Akizungumzia kikosi chao hasa upande wa usajili alisema kuwa tayari wamepokea taarifa kutoka kwa kocha pamoja na mapendekezo ya usajili katika nafasi anazohitaji.

"Kocha ameondoka kwenda kwao Malawi kwenye mapumziko ila ametuachia taarifa yake na mambo anayohitaji hivyo kuanzia Jumatatu tutaanza kushughulikia," alisema  Kimbe. 

Tayari Phiri aliwahi kuidokeza BOIPLUS kuwa katika usajili wake amewapendekeza wachezaji wanne ambao ni Abraham Chove, Paul Ngalema, Hood Mayanja pamoja na  Titto Okelo huku straika Leonard Tsipa kutoka Caps United ya Zimbabwe naye akiwa kwenye rada zake.

Post a Comment

 
Top