BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
BEKI wa Stand United, Joseph Owino ameamua kuachana na timu hiyo ili awe huru baada ya uongozi kushindwa kumlipa haki zake.

Hivi karibuni beki huyo alikwenda Uarabuni ambako alipata timu ya Fanja FC na kusaini mkataba wa miaka miwili lakini uongozi wa Stand United ulimuwekea ngumu wakitaka walipwe kwanza dola 8500 zilizodaiwa kuwa ni kwa ajili ya kibali cha kufanya kazi nchini pamoja na kibali cha makazi walivyomlipia alipotua Shinyanga.

Uongozi wa Fanja uliamua kuachana na Owino aliyelazimika kurejea kwenye kikosi chake ambako hadi sasa hajalipwa pesa yake ya usajili Sh 10 milioni. Owino alisaini mkataba wa mwaka mmoja Stand United akitokea SC Villa.

Owino aliiambia BOIPLUS kuwa maisha ndani ya Stand United yamekuwa magumu kwake hasa baada ya kutolipwa pesa za usajili ikiwemo mishahara hivyo ameomba kuvunja mkataba na timu hiyo.

"Mipango yangu ilizuiwa na wao, pesa za usajili sijalipwa ni bora wangeniacha nicheze Fanja. Matarajio yangu ya kwenda Stand hayakuwa kama nilivyoyafikiria awali hivyo ni bora nikabaki huru, nimeomba waniache huru," alisema Owino.

Msemaji wa klabu hiyo, Deo Makomba alikiri kuwepo kwa mazungumzo baina yao na mchezaji huyo ili waweze kuvunja mkataba wake ili awe huru kufanya mambo yake.

Kocha wa zamani wa Stand United, Patrick Liewig alisikitishwa na kitendo cha Owino kuzuiwa kwenda Fanja akidai kuwa aliruhusu mchezaji huyo aondoke.


Bofya HAPA kusoma stori zaidi za michezo na burudani

Post a Comment

 
Top