BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
TIMU za Geita Gold na Polisi Tabora zimeshushwa hadi ligi ya Wilaya baada ya kukaidi kufanya usajili kwa njia ya mtandao yaani Transfer matching System (TMS) kwenye dirisha la usajili lililopita.

Geita na Polisi zilishushwa hadi ligi daraja la pili baada ya kukutwa na hatia ya kupanga matokeo ya ligi daraja la kwanza na kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA timu zinazoshiriki ligi kuu, ligi daraja la kwanza na la pili lazima zifanye usajili kwa njia ya TMS.

Ofisa Habari wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Alfred Lucas alisema timu hizo zimejishusha zenyewe daraja baada ya kushindwa kufanya usajili kwa njia ya mtandao huku wakijua kuwa walitakiwa kufanya hivyo kama timu nyingine zilivyofanya.

"Natangaza rasmi kuwa timu za Geita na Polisi Tabora zimeshushwa kutoka ligi daraja la pili hadi ligi ya Wilaya kutokana na kushindwa kufanya usajili kwa njia za TMS ambapo kwa kufanya hivyo wamevunja kanuni za FIFA na sisi TFF tunafuata maamuzi toka huko," alisema Lucas.

Kwa maana hiyo timu hizo zina kazi kubwa ya kufanya kama wanataka kucheza ligi kuu kwani wanatakiwa kuvuka madaraja manne ili kufika ambapo itachukua miaka mitano ikiwa itafanya vizuri kila hatua na endapo zitashindwa zitasubiri kwa miaka mingi zaidi.

Tayari timu hizo zilikata rufaa kupinga adhabu hiyo ya kushushwa hadi daraja la pili ambapo hadi sasa rufaa yao imekuwa ikipigwa danadana na TFF.

Post a Comment

 
Top