BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda
STRAIKA wa KRC Genk na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta leo ametimiza siku 76 tangu aifungie klabu yake hiyo bao, lakini unajua amesemaje?, "Mipango ya Mungu tu, hakuna tatizo lolote."

Samatta alikuwa akijibu swali la mwandishi wa BOIPLUS aliyetaka kujua sababu za mkali huyo wa mabao kupotea kwenye orodha ya wafungaji wenye mabao mengi katika ligi kuu ya Ubelgiji na ile ya Europa.

"Kiafya niko poa kabisa na ninayoyafanya sasa ndiyo yale yale niliyokuwa nikifanya zamani, lakini nashangaa sicheki na nyavu.

"Acha nizidi kupiga tizi tu, ipo siku yatarudi mabao yangu, hii ni mipango ya Mungu mwenyewe na kwenye soka haya mambo yapo sana," alisema Samatta ambaye juzi alishindwa kuinusuru timu yake isipate kipigo mbele ya Athletic Bilbao mechi ambayo walipoteza kwa kufungwa mabao 5-3.


Ikumbukwe Samatta alipata majeraha ya goti yaliyomweka nje kwa takribani wiki mbili kabla hajaanza kupewa dakika chache uwanjani na katika mchezo wa juzi dhidi Bilbao alianzishwa kwenye kikosi cha kwanza huku akionyesha kiwango cha juu ingawa bado mabao yalimkataa.

Mashabiki wa Genk wameishuhudia timu yao ikicheza mechi 14 bila kuona nyota huyo wa zamani wa Simba na TP Mazembe akicheka na nyavu ingawa bado mapenzi yao yapo pale pale hasa wakiyakumbuka mabao yake mawili aliyofunga dhidi ya Lokeren Agosti 21 katika ushindi wa mabao 3-0 wakiwa ugenini.

Genk inayoshika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi kuu kwa kujikusanyia pointi 20 kesho inatarajiwa kupambana na Club Brugge katika mchezo wa ligi hiyo inayoongozwa na Zulte Waregem (27) wakifuatiwa na Anderletch na Oostende zenye alama 24 kila moja. 

Post a Comment

 
Top