BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally
ALIYEKUWA Spika wa tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta amefariki dunia usiku wa jana nchini Ujerumani alikokuwa akipata matibabu.

Mbali na mambo yake ya kisiasa na ya kiserikali, Marehemu Sitta (74) alikuwa ni mdau mkubwa wa michezo huku akiwa mwanachama na shabiki wa Simba pamoja na mpira wa kikapu aliowahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Kikapu zamani BATA miaka ya 1974 chini ya Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu, Agustino Ramadhani.

Serikali na familia ya michezo nchini imepokea kwa mshituko mkubwa kifo cha Mheshimiwa Sitta mzaliwa wa Urambo, Tabora huku Klabu ya Simba ikiwa kwenye msiba mkubwa kwani kiongozi huyo alikuwa ni mdhamini mwandamizi wa Simba tangu miaka ya nyuma.

Baraza la Wadhamini la Simba, liliundwa na Marehemu Sitta ambaye alikuwa mwanachama wa tawi la Mpira Pesa lenye maskani yake Magomeni, jijini Dar es Salaam akiwa ni mwanachama mwenye kadi namba moja, wengine waliopo kwenye baraza hilo ni Mwenyekiti wa zamani, Hassan Dalali, Ramesh Patel na Adam Mgoyi.

Kwa upande wa familia ya mchezo wa kikapu nchini, imepata pigo kubwa kwani mchango wake hasa ulionekana pale ambapo chama hicho kilipoteza mwelekeo na kufa kabisa ambapo kwa jitihada zake na mwenzake, Jaji Agustino walifanikiwa kukifufua chama hicho mwaka 1972.


Jaji Augustino Ramadhan

Jaji Agustino amepokea kwa mshituko mkubwa taarifa za kifo cha mtendaji wenzake na kusema kwamba; "Hili ni pigo, nimeshtuka sana, wakati huo mimi ni Mwenyekiti yeye alikuwa Makamu Mwenyekiti, tulifanya kazi kwa kushirikiana kuhakikisha mpira wa kikapu unakuwa taa ndani ya nchi. Wote tuliupenda mchezo huo ndio maana tulikuwa na nia.

"Sitta alicheza mpira wa kikapu wakati anasoma Tabora, baadaye alipopata kazi hata mimi nilihamishiwa huko Tabora. Chama cha Mpira wa Kikapu nchini (BATA) kilikuwa kimekufa kabisa ndipo tulipoamua kukifufua, kikao chetu cha kufufua chama kilifanyika Iringa. Alikuwa na mchango mkubwa kwa kweli na chama chetu kilisimama imara mpaka tulipowakabidhi wengine," alisema Jaji Agustino.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini, Richard Kaselela aliyewahi kuwa Rais wa TBF (Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania) ambalo zamani iliitwa BATA, alisema kuwa; "Binafsi si pigo tu kwenye michezo kwani yule ni kama baba yangu, amezaliwa mwaka mmoja na baba yangu na wamesoma shule moja Tabora Boys, walikuwa marafiki wakubwa hivyo familia zetu zinaishi kama ndugu.

"Marehemu Samuel Sitta kwanza alikuwa ni mdau wa Simba, nawapa pole sana Simba lakini kwenye kikapu huku aliweza kumaliza kila kitu, alitushauri na kutoa msaada ni pigo kila sehemu, tuliondokewa na mzee Mlaya, Mwamlenga ambao wote walikuwa na uchungu na kikapu ila kwasasa kikapu kinashuka kwani wenye busara wanazidi kutwaliwa na Mungu.

"Nawataka wanakikapu kujitokeza kwa wingi kwenye safari ya mwisho ya kiongozi wetu huyu, ikiwezekana kusaini mpira wa pamoja kama kumbukumbu kwa familia kutokana na mchango alioutoa kwetu," alisema Kasesela.


Mdhamini na mtatua migogoro Simba
Dalali ameelezea kwamba wamepoteza mtu muhimu ndani ya Simba ambaye hawajui wataziba vipi pengo lake, kwani hata pale mgogoro unapotokea kimbilio la kwanza kupata usuluhishi ni kwa Marehemu Sitta.

"Nashindwa kuelezea, sijui nimwelezee vipi Samuel Sitta, ila ameacha pengo kubwa ndani ya Simba, alikuwa mtu muhimu sana kwetu. Tukiwa na migogoro ya klabu basi mtu wa kwanza na aliyefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuimaliza hiyo ni Samuel Sitta, amefanya kazi nyingi na ngumu za klabu ya Simba.

"Ukiachana na hayo majukumu ambayo ni makubwa na mazito, Marehemu Sitta alikuwa mdhamini wetu wa miaka na miaka, ameisadia Simba kiasi kwamba huwezi kuhesabu, hakika imezimika nyota muhimu na kali kwetu, ni pigo na ni msiba mkubwa kwa Wanasimba, ila hatuwezi kupingana na majukumu ya Mungu," alisema Dalali.

Aipeleka Simba Brazil
Dalali anasimulia zaidi; "Mchango wa Marehemu Sitta ndani ya Simba ulianza kuonekana kuanzia miaka ya 70, Sitta aliipeleka Simba nchini Brazil ilikopiga kambi ya miezi mitatu ikiwa ni maandalizi ya ligi kuu mwaka 1982, wakati huo ni Waziri wa Ujenzi, inauma sana, tumempoteza msuluhishi wetu, mtu mwenye msaada mkubwa ndani ya Simba,".

Mwenyekiti wa Tawi la Mpira Pesa, Ustadhi Masoud naye alikuwa na haya; "Marehemu alikuwa mwanachama wetu wa kwanza kwa maana mwanachama kadi namba moja, amelisaidia tawi letu kwa kiwango kikubwa na kutupa jeuri hii, leo hii Mungu amefanya mapenzi yake. Ila ukweli ametuacha katika wakati mgumu na pengo lake ni kubwa,".

Post a Comment

 
Top