BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
SERIKALI imetoa baraka zake katika Mkutano mkuu wa dharura wa klabu ya Simba wa mabadiliko ya Katiba uliopangwa kufanyika kwenye Bwalo la maafisa wa Polisi Osterbay Disemba 11 ikiwa utafuata taratibu kwa mujibu wa katiba yao.

Jana Uongozi wa Simba ulitangaza Mkutano mkuu wa dharura kwa ajili ya marekebisho ya Katiba ambayo kwa kauli moja yatapitisha suala la uendeshwaji kwa mfumo wa hisa ambapo mfanyabiashara Mohamed Dewji 'MO' amepanga kununua hisa za asilimia 51.

Katibu mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja amewaambia Waandishi wa Habari kuwa endapo Mkutano huo utafuata taratibu zote kwa mujibu wa Katiba ya klabu hiyo Serikali haitakuwa na pingamizi lolote.

Kiganja alisema kuwa kama hakuna malalamiko kutoka kwa wanachama wao na muda ni mrefu kabla ya Mkutano huo kufanyika utaratibu umefuatwa basi wao wanaubariki wala hawana pingamizi kwa Wekundu hao.

"Serikali ipo kwa ajili ya kuongoza michezo yote nchini na kujipanga kwa kila hali kuhakikisha migogoro isiyo ya lazima inaepukwa hususani klabu za Simba na Yanga ambazo zina mashabiki wengi" alisema Kiganja.

Miezi kadhaa iliyopita Kiganja alipiga marufuku michakato yote ya kiundeshwaji kwa klabu hizo kongwe nchini hadi utaratibu utakapo fuatwa kwa mujibu wa Katiba zao.

Post a Comment

 
Top