BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Shinyanga
SIMBA 4G haikamatiki! Ndio kauli pekee ambayo unaweza kuielezea kasi ya timu ya Simba baada ya kushinda michezo 11 na kutoka sare miwili kisha kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi ya Vodacom kwa kufikisha pointi 35.

Simba imevunja mfupa uliozishinda timu za Yanga na Azam baada ya kuichapa bao 1-0 Stand United kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga na sasa kuwa mbele kwa tofauti ya pointi 8 na Mabingwa watetezi ya Yanga wanaoshika nafasi ya pili.Stand kwa nyakati tofauti ilizifunga timu za Azam na Yanga bao 1-0 katika dimba hilo hilo lakini leo imekuwa tofauti baada ya kukubali kichapo kutoka kwa Mnyama Simba.

Shiza Kichuya ndiye aliyefunga bao hilo la ushindi kwa mkwaju wa penalti dakika ya 32 baada mshambuliaji Laudit Mavugo kuangushwa kwenye eneo la hatari na bila ajizi mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar aliutumbukiza mpira kimiani na kuendelea kuwa kinara wa ufungaji baada ya kufikisha mabao tisa hadi sasa.Kiungo Musa Ndusha aliichezea Simba mechi yake ya kwanza ya ligi kuu tangu asajiliwe baada ya kuingia uwanjani dakika ya 78 kuchukua nafasi ya Mwinyi Kazimoto. Ndusha amepata Hati yake ya Kimataifa ya Uhamisho wiki moja na nusu iliyopita ambayo ilikuwa ikimfanya ashindwe kuwatumikia Wekundu hao wa Msimbazi.

Matokeo mengine ya mechi zilizochezwa Leo

Mbeya City 2-1 Yanga
Ruvu Shooting 1-0 African Lyon
Toto African 0-1 Azam FC
Ndanda FC 1-0 Prisons

Post a Comment

 
Top