BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
BEKI wa timu ya Simba, Abdi Banda na uongozi wa timu hiyo ni kama wamewekeana mtego wa nani aanze kuvunja 'ndoa' yao kabla ya Mei mwakani ambapo mkataba wa mchezaji huyo na Simba unamalizika.

Tangu msimu huu uanze, Banda aliyesajiliwa na Simba akitokea Coastal Union hajapata nafasi ya kucheza mara kwa mara huku akipewa matumaini kuwa atapangwa kwenye mechi zijazo za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Kuna habari kwamba benchi la ufundi chini ya Kocha Mcameron, Joseph Omog wamependekeza kuwa Banda na wenzake Awadh Juma, Hija Ugando na Manyika Jr wapelekwe kwenye timu nyingine kwa mkopo kwani hawamo kwenye mipango yake.

Uchunguzi uliofanywa na BOIPLUS umebaini kuwa beki huyo hana furaha na maisha ndani ya Simba kwani hana uhakika wa kupata namba na ndio maana ameonyesha nia ya kutaka kuvunja mkataba japokuwa viongozi wa timu hiyo hawataki kuvunja ndoa hiyo.

Banda mwenye uwezo wa kucheza kwa ufasaha nafasi zote za ulinzi lakini pia kama kiungo mkabaji alishindwa kuaminiwa na makocha wake katika kikosi cha Simba mbele ya wachezaji waliopo sasa akiwemo Mohamed Hussein 'Tshabalala' na Jonas Mkude.

Banda ameiambia BOIPLUS kuwa amewasiliana na uongozi wa Simba kuhusu suala hilo la kuvunja mkataba ambapo mpaka mwisho wa wiki hii kila kitu kitakuwa sawa.

"Ni kweli navunja mkataba na Simba kuna vitu vidogo havijakamilika lakini muda si mrefu kila kitu kitakuwa hadharani," alisema Banda.

Meneja wa mchezaji huyo, Abdul Bosnia alisema kuwa, "Banda anaumia kukaa pasipo kucheza na hizi taarifa za kutolewa kwa mkopo ni kumshusha thamani, mazungumzo yetu ya awali hatukufikia hatua hiyo kwani walisema bado wanahitaji huduma yake.

"Hivyo tunasubiri kama ni kweli wanataka apelekwe kwa mkopo itabidi tuzungumze upya ili tukubaliane kuvunja mkataba ili awe mchezaji huru nadhani kila kitu kitajulikana siku zijazo, Banda hajapeleka barua ila alikusudia hivyo maana ameumia, ni kama anachukuwa mshahara pasipo kufanyakazi," alisema Bosnia.

Imeelezewa kuwa beki huyo ana matarajio makubwa ya kupata timu nyingine kama Simba wataafikiana kuvunja mkataba katika nchi ya Afrika Kusini, Kenya na hapa hapa Tanzania.

Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu alisema kuwa hawana taarifa wala kupokea barua ya maombi y kuvunja mkataba kutoka kwa Banda ikifika wataijadili.

Post a Comment

 
Top