BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

UONGOZI wa klabu ya Simba umesema hautacheza mchezo wowote wa ligi dhidi ya watani wao wa jadi Yanga endapo waamuzi hawatoka nje ya nchi tena wenye uzoefu wa mechi kubwa wanaotambuliwa na FIFA.

Simba wako tayari kulipa gharama za waamuzi hao kuanzia mwamuzi wa kati na wasaidizi wake wawili ili haki itendeke kwakua watani wao wamekuwa wakipendelewa mara kwa mara na marefarii wa hapa nchini.

Msimamo huo umetolewa na msemaji wa klabu hiyo Haji Manara alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari klabuni hapo na kusema kuwa kwa sasa hawatakuwa tayari kuona haki zao zikidhulumiwa kwa namna yoyote na wataanzia mzunguko wa pili unaotarajiwa kuanza Disemba 17.

"Simba haitacheza mechi yoyote dhidi ya Yanga ikichezeshwa na waamuzi wa nyumbani, tupo tayari kulipa gharama zote za kuwaleta marefarii kutoka nje ya nchi ili kuepuka hujuma za watani wetu.

"Kila mtu aliona jinsi mwamuzi Jonensia Rukyaa alivyotunyonga msimu uliopita na Martin Saanya mechi iliyopita sasa hatuwataki maamuzi wote wa Tanzania kwenye mechi dhidi ya Yanga. Mechi ya Zamelek na Al Ahly waamuzi wanatoka nje ya Misri na sisi tunataka hivyo" alisema Manara.

Wakati huo Manara ameishangaa Kamati ya masaa 72 ya Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF kuendelea kufanya uchunguzi juu ya sakata la Saanya na Samwel Mpenzu wakati mengine tayari wametoa maamuzi na adhabu pia.

"Tangu mchezo wetu na Yanga hadi leo ni siku 53 zimepita lakini bado uchunguzi unaendelea makocha wa Yanga na Azam, timu  pamoja na wachezaji waliofanya makosa mzunguko wa kwanza wamepata adhabu kwanini suala la Saanya hadi leo linasubiri uchunguzi?" alihoji Manara.

Post a Comment

 
Top