BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
NI takribani saa 18 tu zimebaki Simba kuivaa African Lyon, mechi itakayopigwa Uwanja wa Uhuru na baada ya mechi hiyo keshokutwa Jumatatu asubuhi Wekundu hao wa Msimbazi watakwea pipa (Ndege) kuifuata Prisons jijini Mbeya.

Simba watafunga mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa kukutana na maafande hao wa Magereza kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Novemba 10 huku wakiwa na mtaji mzuri mkononi wa pointi 35 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote katika mzunguko huu.

Hiyo inamaanisha kwamba Simba watakwenda kula sikukuu ya Krismasi roho zao zikiwa na furaha huku wakienda kukusanya nguvu mpya kwa ajili ya mechi za mzunguko wa pili utakaoanza Desemba.

Simba inaingia dimbani ikiwa imetokea Kanda ya Ziwa walikokuwa na mechi mbili dhidi ya Mwadui na Stand United ambazo walishinda zote hivyo kukusanya pointi sita na sasa kwenye ukanda huo wamebakiza mechi tatu dhidi ya Toto African, Mbao na Kagera Sugar zitakazochezwa mzunguko wa pili.Safari ya kwenda Kanda ya Ziwa kwa timu hiyo ilianzia Uwanja wa Ndege wa Mwalimu JK Nyerere baada ya kufanya vizuri mechi zao zote 13 walizocheza na kuwapa matumaini mapya wanachama, mashabiki na viongozi ya kuweza kutwaa ubingwa wa VPL ambao hawajaupata kwa miaka minne sasa.

Uongozi wa Simba umeangalia ratiba ya ligi ilivyopangwa na kuona kwamba itawaumiza wachezaji wao na kupoteza mechi kama tu watatumia usafiri wa barabara hivyo waliamua kuanza kuingia mifukoni na kusafirisha kikosi chao kwa Ndege.

Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu alithibitishia BOIPLUS juu ya safari hiyo kwamba kikosi chao kitaondoka na Ndege ya Fastjet keshokutwa asubuhi ili kupata muda wa kujiandaa.

Post a Comment

 
Top