BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar

SIMBA imempa mkataba wa miaka miwili beki wao Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' lakini ndani ya mkataba huo unakutana na kipengele kigumu cha kuvunja mkataba endapo beki huyo atapata timu nyingine hapa hapa nyumbani.

Kipengele hicho kinasema timu ambayo itamuhitaji mchezaji huyo ama kama mchezaji mwenyewe atataka kuvunja mkataba na kwenda timu nyingine ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) basi atalazimika kuilipa Simba dola 600,000 sawa na zaidi ya Sh 1.2 bilioni. 

Klabu za VPL hakuna ambayo inaweza kulipa pesa hiyo labda matajiri wa ligi Azam FC na Yanga ndio pekee wanaoweza kujaribu kuvunja mkataba huo na si vinginevyo ingawa ni wazi kwamba unazibana timu nyingine kumpata Zimbwe Jr. Yanga ndiyo timu iliyokuwa ikitajwa kumnasa beki huyo kabla hajaongezwa mkataba huo.

Katika mikataba ya wachezaji wa Simba kipengele hicho kipo kwa kila mchezaji ingawa wapo walioondoka na kutolipa pesa hiyo kwani Simba wao walikiuka baadhi ya vipengele kwa kushindwa kutimiza makubaliano yao kwa wachezaji akiwemo Ramadhan Singano aliyetimkia Azam ambaye alidai kuwa Simba wamevunja mkataba wake kwa kushindwa kumlipia pango.


Mkataba wa Singano nao ulikuwa ukielezea kwamba akivunja atalazimika kuilipa Simba dola 600,000 vivyo hivyo kwa beki Hassan Kessy aliyekwenda Yanga ambapo hadi sasa Simba wamekomalia walipwe pesa hiyo kwani Yanga walimsainisha mchezaji wao kimakosa akiwa bado ana mkataba.

Habari zaidi kuhusu Zimbwe Jr, aliyesaini mkataba huo jana wenye thamani ya Sh 40 milioni, zinasema kuwa uongozi wa Simba umempa uhuru kwamba akipata timu nje ya nchi basi watakuwa tayari kumuuza hata kwa dola 80,000.

Meneja wa mchezaji huyo Herry Mzozo aliiambia BOIPLUS kuwa, "Ulileta utata kidogo ila wamekataa kubadilisha hicho kipengele lakini akipata timu nje ya nchi itakuwa rahisi kuliko timu za hapa hapa,".

Post a Comment

 
Top