BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
MSIMU uliopita kwenye Uwanja wa Sokoine kulikuwa na ukame mkubwa wa mapato ingawa Yanga ndio waliujaza zaidi uwanja huo. Mapato ya juu msimu huo yalikuwa ni mechi ya Yanga na Mbeya City iliyoingiza Sh 50 milioni.

Ni mapato mekubwa ila msimu huu Simba ilienda kwenye uwanja huo huo kucheza na Mbeya City na kuvunja rekodi ya msimu uliopita wa Yanga kwani waliingiza Sh 60 milioni mapato ambayo yameshindwa kuvunjwa na watani zao hao walipocheza jana Jumatano na City.

Simba ilishinda mechi hiyo kwa mabao 2-0 wakati Yanga walioingiza Sh 35.7 milioni walichezea kichapo cha mabao 2-1 na Wagonga Nyundo hao.

Lakini rekodi zinaonyesha pia kwamba mjini Shinyanga bado Simba imefanya vizuri kwani Yanga walipocheza na Stand United waliingiza Sh 33.7 milioni huku Simba yenyewe ikiingiza Sh 45.8 milioni na kufanya iwe imeingiza jumla ya Sh 105.8 milioni kwa mechi mbili wakati Yanga jumla yake ni Sh 69.4 milioni.

Simba ambayo ina pointi 35 imeizidi Yanga kwa Sh 36.4 milioni pamoja na pointi nane kwani wao wamekusanya pointi 27 wakishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.

Msimu uliopita Simba ilikuwa ikilalamika juu ya mapato yao kushuka yakisababishwa na sababu mbili mashabiki kutokwenda uwanjani kutokana na timu yao kufanya vibaya pamoja na kuangalia mechi zao kwenye televisheni jambo ambalo linawakuta Yanga kwasasa kwani timu yao haifanyi vizuri.

Post a Comment

 
Top