BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Mbeya
SIMBA imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa maafande wa Magereza (Prisons) mchezo uliofanyika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Huu ni mchezo wa pili mfululizo kwa kupoteza kwani mechi iliyopita kabla ya kukwea pipa walifungwa bao 1-0 na African Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru hivyo wamewazidi watani zao Yanga kwa pointi tano peeke kwani Simba ipo kileleni ikiwa na pointi 35 wakati Yanga ambao watacheza kesho na Ruvu Shooting wakishika nafasi ya pili kwa pointi 30.

Kwa matokeo hao Simba wanaanza kupunguza kasi waliyoanza nayo kwani kama Yanga watashinda mechi ya kesho Alhamisi basi watazidiwa pointi mbili pekee ila wakipoteza mechi hiyo bado watakuwa na kazi nzito ya kuwafukuzia Wekundu hao wa Msimbazi.

Kocha wa Prisons, Meja mstaafu Abdul Mingange aliingia na mbinu ya kuzuia zaidi huku wakifanya mashambulizi yakushtukiza wakati Simba wakitawala sehemu kubwa ya mchezo wakitumia zaidi pembeni kwa mawinga wao.

Jamal Mnyate aliifungia Simba bao la kwanza kwa kichwa dakika ya 43 baada ya kumalizia krosi safi iliyopigwa na winga Shiza Kichuya upande wa kushoto wa Uwanja.


Prisons walirudi kwa kasi kipindi cha pili ambapo dakika ya 47 Victor Hangaya aliisawazishia kwa kichwa baada ya mabeki wa Simba kushindwa kuondoa hatari huku mlinda mlango Vicent Angban akiwa hana lakufanya.

Hangaya tena aliipatia Prisons bao la pili dakika ya 63 kwa kichwa alimalizia mpira wa kona ambao kwa mara nyingine mabeki wa Simba wakishindwa kujipanga na kumuacha mshambuliaji huyo mwenye kimo kirefu kuruka bila kukabwa.

Mchezo mwingine Azam wameibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Mwadui FC mchezo uliofanyika Uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga. Azam wamemaliza mzunguko wa kwanza kwa kukusanya pointi 25 wakishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakati Mwadui wao wana pointi 13 nafasi ya 15.

Mzunguko wa kwanza wa ligi utamalizika kesho kwa mchezo mmoja utakaofanyika  Uwanja wa Uhuru kati ya Yanga na Ruvu Shooting.

Post a Comment

 
Top