BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
TIMU za Simba na Yanga zimefikia makubaliano ya kulipana fidia kuhusu mkataba wa beki Hassan Kessi na suala hilo linatarajiwa kumalizika wikiendi hii.

Kwa muda mrefu sasa suala hilo limekuwa likibeba vichwa vya Habari mbalimbali baada ya beki huyo kusaini Yanga huku mkataba wake na Simba ukiwa bado haujamalizika.

Jana jioni Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji iliketi  pamoja na msuluhishi Mzee Saidi El Maamry na wawakilishi wa Klabu hizo na kufikia muafaka ambapo suala hilo linatarajiwa kumalizwa Wikiendi hii.

Ofisa Habari wa Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Alfred Lucas alisema pande zote zilikutana jana jioni kwa ajili ya kulimaliza kabisa suala hilo na kwamba makubaliano yamefikiwa na Simba italipwa fidia.

"Kuhusu Suala la beki Hassan Kessi limefikia hatua nzuri pande zote zilikutana jana mbele ya Kamati na msuluhishi Mzee El Maamry na kwasasa naweza kusema limemalizika kwa kiasi kikubwa," alisema Lucas.

Awali Simba waliitaka Yanga kuwalipa kiasi kikubwa cha fedha kwa kumsajili beki huyo pasi na kufuata utaratibu lakini baada ya kuketi pamoja Wekundu hao wakalegeza kidogo Uzi ili suala hilo liweze kumalizwa.

Endapo pande zote zingeshindwa kufikia muafaka suala hilo lingerudishwa kwenye Kamati hiyo kwa ajili ya kufanyiwa maamuzi kwa mujibu wa kanuni za TFF.

Post a Comment

 
Top