BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu

KAMATI ya masaa 72 ya shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) imesema uchunguzi dhidi ya waamuzi Martin Saanya, Samuel Mpenzu (mechi ya Yanga Vs Simba), Thomas Mkombozi (mechi ya Coastal Union Vs KMC) na Rajab Mrope (mechi ya Mbeya City na Yanga) umekaribia kukamilika.

Hatua ya mwisho ya uchunguzi huo  wanatakiwa kufika mbele ya Kamati hiyo  ambapo watahojiwa ili kutoa ufafanuzi katika masuala mbalimbali yaliyojitokeza katika taarifa zao.

MATUKIO YA LIGI KUU
Mchezo namba 90 (Simba Vs Toto Africans). Klabu ya Toto Africans imepewa onyo kali kutokana na timu yake kuchelewa kufika uwanja kwa dakika saba. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.

Mechi namba 99 (Mwadui Vs Simba). Klabu zote mbili zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kuingia uwanjani kwa kutumia mlango wa mashabiki, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48).

Mechi namba 101 (Ruvu Shooting Vs Stand Utd). Ndanda FC imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48).

Nayo Ruvu Shooting ambayo ilikuwa uwanja wa nyumbani, imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 15. Kitendo hicho ni ukiukwaji wa Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu, na adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48).

Mechi namba 104 (JKT Ruvu Vs Ndanda). Klabu ya Stand United imepewa onyo kali baada ya wachezaji wake kufanya vurugu wakitaka kuingia uwanjani bila ya kuwa na uthibitisho kuwa wao ni wachezaji wa timu hiyo wakati wa mechi kati ya JKT Ruvu na Ndanda iliyofanyika Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 42(1).

Mechi namba 112 (Majimaji Vs JKT Ruvu). Daktari wa JKT Ruvu, Abdullah Yusuf amefungiwa miezi mitatu, na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kusababisha usumbufu kwa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, na kuwatolea maneno machafu Mwamuzi na Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 41(2).

Mtaalamu wa viungo wa JKT Ruvu, George Minja amefungiwa miezi mitano na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kumvamia Mwamuzi akitaka kumpiga, na pia kutoa lugha ya matusi kwa waamuzi baada ya mechi hiyo. Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41(2).

Nao wachezaji wa JKT Ruvu, Said Kipao, Samwel Kamuntu, Pela Mavuo na Paul Mhidzhe wamefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa kuwatukana waamuzi baada ya mchezo kumalizika. Adhabu imezingatia Kanuni ya 37(7).

Mechi namba 116 (Mbao FC Vs Azam FC). Kocha wa Azam FC, Zeben Hernandez amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi kwa kukataa kuheshimu mipaka ya eneo la ufundi  katika mechi hiyo. Adhabu imezingatia Kanuni ya 40(11).

Mechi namba 117 (Ndanda Vs Stand Utd) Katika mechi hiyo kadri muda ulivyokuwa ukienda ball boyz walichelewesha kurudisha mipira uwanjani, na mbaya zaidi mipira ilikuwa ikifichwa kiasi cha kubaki miwili kati ya sita iliyokuwepo. Msimamizi wa Kituo ameandikiwa barua ili ahakikishe suala hilo halijitokezi tena.

Mechi namba 59 (Yanga Vs Ruvu Shooting). Timu ya Ruvu Shooting imepewa onyo kali kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 12, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu.

Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu baada ya wakati wa mapumziko kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa. Pia baada ya mechi kumalizika alikwenda kwenye chumba cha waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa. Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 40(1).

Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya washabiki wake kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa walipokuwa wakiingia vyumbani wakati wa mapumziko. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1).

Mechi namba 60 (Tanzania Prisons Vs Simba). Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na timu yake kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi  na kufika wakati taratibu zote za msingi zikiwa zimemalizika

Post a Comment

 
Top