BOIPLUS SPORTS BLOG


Karim Boimanda
UNAHITAJI zaidi ya masaa matatu kutoka Dar es Salaam hadi Johannesburg nchini Afrika Kusini kwa usafiri wa ndege, akina sisi ambao ndege kwetu ni habari nyingine tunaweza kuomba kushushwa njiani tupumzike kidogo na kuchimba dawa.

Lakini watu hawana huruma bwana, kuanzia Oktoba 25 hadi leo hii Bodi ya Ligi imeisafirisha Stand United kutoka Dar hadi Johannesburg na kurudi Dar tena kwa basi, kisa nini?, kujiita Wapiga Debe, ama!

Watu wengi walishapaza sauti kuhusu upangaji mbovu wa ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom lakini hakuna mabadiliko yoyote, tena msimu huu hali ndio imekuwa mbaya zaidi. Naamini TFF na Bodi ya ligi mnapaswa kukubali kuwa ubora wa ligi huanzia kwenye ratiba, hebu basi orodhosheni hizi changamoto mje kuzifanyia kazi mtakapopanga ratiba ya msimu ujao.


Timu nyingi zimeathiriwa na ratiba hii mbovu lakini hawa Stand jamani wanatia huruma, nilianza kufuatilia safari zao tangu Oktoba 25 walipoifunga Yanga bao 1-0 pale Shinyanga kabla hawajasafiri Km 1,203 kuifuata Majimaji mjini Songea ambako pia walifanikiwa kujizolea alama tatu kwa kuwafunga wanalizombe mabao 2-0.

Stand wanaoshika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia pointi 22 walisafiri tena Km 477 hadi Mbeya ambako walitoka suluhu na Mbeya City, hiyo ilikuwa Oktoba 7 halafu wakarejea Shinyanga ambako ni umbali wa Km 759 kutoka Mbeya.

Wakiwa mjini Shinyanga, Wapiga Debe hao ambao ndoa yao na Acacia ilivunjika miezi michache iliyopita, walicheza mechi mbili ambapo walifanikiwa kuifunga Azam FC bao 1-0 kabla hawajatoka sare ya bao moja na African Lyon. Unajua kilichofuata?, walilazimika kurejea tena Mbeya kuifuata Prisons.Tangu wapate ushindi dhidi ya Azam, Stand hawajawahi kushinda tena na wakitoa sababu ya uchovu mimi mzee wa Black & White nitakuwa upande wao. Stand iliyoshinda dhidi ya Yanga na Azam si Stand iliyopigwa 2-1 na Prisons kule Mbeya.

Kuyumba kwao kulidhihirika pale walipoitangulia Mtibwa na baadae wakata miwa hao wakarudisha mabao yote na kutoka sare ya mabao matatu. Kumbuka walikuwa wametoka Mbeya ambako ni umbali wa Km 728 huku wakisubiriwa kusafiri Km 329 zingine kuifuata Ruvu Shooting walikoenda kuambulia suluhu Oktoba 30.

Alfajiri ya siku iliyofuata Stand walianza safari ya kurejea mjini Shinyanga kuvaana na Mnyama Simba ambaye msimu huu ndio haambiwi wala hasikii linapokuja suala la pointi tatu, amekuwa mtata kweli kweli, labda ni kweli haya wanayosema kitaa kuwa 'Mnyama kamisi kukwea pipa'. 


Umbali wa kutoka Mlandizi hadi Shinyanga ni Km 916, walipofika kule Stand walisikika wakijinadi kuwa hawajachoka na wapo tayari kupambana, lakini ni kwavile tu hawakuwa na jambo jingine la kuongea ambalo lingewapa motisha, ila ukweli walikuwa wanaujua wenyewe. Mnyama akajipigia kimoja kisha kukwea pipa akiwa na pointi zake tatu muhimu.

Muda huu ninaandika makala hii Wapiga debe hao sijui wapo stendi gani wakielekea mjini Mtwara kuifuata Ndanda FC ili kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi ambapo kama wakishinda watafikisha alama 25 za machozi, jasho na damu.

Ndani ya siku 43, Stand watakuwa wamecheza michezo tisa lakini ni baada ya kusafiri umbali wa Km 8,202 ambazo ni takribani sawa na safari ya kutoka Dar kwenda Johannesburg kisha kurudi hadi Shinyanga kwa basi lao lile lililoandikwa 'Chama la Wana'. Mungu anawaona nyie Bodi ya Ligi

Mob; +255788334467
E-mail; karim@boiplusmedia.com

Post a Comment

 
Top