BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
WINGA wa Simba, Shiza Kichuya ndiye anayeongoza kwa ufungaji wa magoli hadi ligi inakwenda mapumziko akiwa na mabao tisa lakini straika wa Yanga, Amissi Tambwe ambaye ana magoli saba ametamka kauli moja tu kuwa kutangulia si kufika.

Kwa kauli hiyo inaonyesha kwamba Kichuya ametangulia tu ila ufungaji bora msimu huu unaweza kuwa wa mchezaji mwingine kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo Hamisi Kiiza ndiye aliyepewa nafasi kubwa ya kuwa Mfungaji Bora lakini Tambwe akampindua baadaye.Msimu uliopita Kiiza aliyeichezea Simba alimaliza ligi akiwa na mabao 17 huku Tambwe akiwa Mfungaji Bora kwa mabao 19 na kabla ya kibao kugeuka Kiiza raia wa Uganda alikuwa amemwacha mbali Mrundi huyo ambaye ametwaa kiatu cha Dhahabu kwa misimu miwili tofauti kwenye ligi ya Tanzania Bara.

Akizungumza na BOIPLUS, Tambwe alisema kuwa, "Kila siku huwa natamani kuwa juu kwa jambo lolote ninalofanya, hivyo msimu unapoanza huwa naweka malengo ya kuwa juu labda itokee tu iwe tofauti, ndiyo maana nasema mwingine anaweza kutangulia ila asiwe wa kwanza kufika. Mechi 15 zilizobaki za mzunguko wa pili ni nyingi sana hivyo bado nina nafasi ya kupambana.


"Kutokana na ugumu wa ligi mzunguko huu wa kwanza ndio unasababisha hata ukame wa mabao, kingine ni mabadiliko ya uwanja pale Taifa uwanja ni mpana na ulitupa nafasi ya kucheza kwa kujiachia na kufunga mabao mengi tofauti na Uhuru, hatuchezi kwa kujiachia na haupo kwenye ubora, hata timu huwa zinapata ushindi wa mabao machache," alisema Tambwe na kuongeza.

"Kuzidiwa mabao mawili hakuwezi kunikatisha tamaa, nitapambana na kuongeza juhudi ili nifikie malengo yangu ya kuwa juu ya wengine wote," alisema.

Tambwe anaondoka usiku wa leo kwenda kwao Burundi kwa ajili ya mapumziko mafupi ambapo Yanga inatarajia kurudi kambini Novemba 28 wakati mzunguko wa pili utaanza Desemba 17.

Post a Comment

 
Top