BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
SERIKALI ya Tanzania itaendeleza ushirikiano baina yake na Serikali ya Afrika Kusini katika masuala mbali mbali yakiwemo Sanaa na Utamaduni.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Nape Nnauye alipotembelewa na Waziri wa  Utamaduni wa Afrika Kusini Nkosinathi Mthehwa ofisini kwake asubuhi ya leo ambapo katika mambo waliyoyazungumza moja wapo ni kushirikiana kwenye masuala ya sanaa na wasanii.

Mwaka 2011 Serikali hizo ziliingia makubaliano ya kufuta viza baina ya wananchi wa pande zote mbili ili kuhakikisha kunakuwa na urahisi wa kusafiri kwa ajili ya kubadilishana uzoefu katika mambo mbali mbali hususani sanaa na wasanii.

Nape alisema Afrika Kusini wameendelea katika masuala ya sanaa hasa miundombinu yao ndiyo maana wasanii wa Tanzania wanaenda nchini humo kutengeneza muziki na kufanya video kwa urahisi ukilinganisha nchi nyingine.

"Wasanii wetu wana uwezo wa kwenda Afrika Kusini kuandaa video zao kwa urahisi kwakua tuna makubaliano tuliyoingia mwaka 2011 na tumepanga kuyaboresha zaidi," alisema Nape.

Kwa upande wake Waziri Mthehwa alisema anatambua umuhimu wa Tanzania katika kuisaidia nchi yake kupata Uhuru ndiyo maana wanafanya mambo mengi pamoja ili kuthamini mchango huo.

Mthehwa alisema pia lengo la nchi hizo ni kuona utamaduni unaenziwa na vijana wa sasa huku akisisitiza tasnia ya filamu inatakiwa kupanda zaidi kama ilivyo nchi za India, Ghana na hata Nigeria.

"Na sisi tunataka tufike kama walivyo wenzetu wa Bollywood (India) na Nollywood (Nigeria) katika masuala ya filamu na kwa pamoja tunaweza kufikia huko," alisema Mthehwa.

Post a Comment

 
Top