BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Dar
BAADA ya Ruvu Shooting kuweka msimamo wao wa kutopeleka timu uwanjani kesho Jumatano kucheza na Yanga, Shirikisho la Soka nchini (TFF) limekubali maombi ya Maafande hao na sasa mechi hiyo itachezwa keshokutwa Alhamisi Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Ruvu walituma maombi yao jana Jumatatu kuomba mchezo huo usogezwe sababu kubwa ni wachezaji wao kuchoka kutokana na safari ya kutoka Bukoba ambapo wametumia siku mbili njiani na kuingia leo saa 4 asubuhi. Ruvu walikwenda kucheza na Kagera Sugar juzi Jumapili.

TFF imejiridhisha kuwa Ruvu Shooting imechelewa kuingia kituo cha Dar es Salaam, ndiyo maana mchezo dhidi ya Yanga umesogezwa mbele.

Michezo mingine ya kesho Jumatano inahusisha timu za Mwadui ya Shinyanga na Azam FC ambayo ilipewa jina la Mechi Na. 57 itachezwa Uwanja wa Mwadui wakati Simba itasafiri hadi Mbeya kucheza na Tanzania Prisons katika mchezon Na. 60 Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine.

Mechi zilipangiwa ratiba, lakini tarehe zake hazikupangwa (TBA). Tayari Bodi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), imewasiliana na wahusika kuhusu mabadiliko hayo.

Sababu ya kuvuta nyuma michezo hiyo ni kutoa nafasi ya maandalizi ya kambi ya timu ya Taifa 'Taifa Stars’ inayotarajiwa kusafiri Ijumaa wiki hii kwenda Harare, Zimbabwe kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa unaotarajiwa kufanyika Novemba 13.

Post a Comment

 
Top