BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
KOCHA wa zamani wa Simba, Patrick Phiri ameifuatilia timu hiyo hatua kwa hatua wakiwemo nyota wao Shiza Kichuya na Mzamiru Yassin na kutamka kuwa vijana hao wanapaswa kuwa na mawazo ya mbali zaidi kama ilivyokuwa kwa Musa Mgosi.

Phiri amechukulia mfano wa Mgosi ambaye ni Meneja wa timu hiyo baada ya kutangaza kustaafu soka kuwa aliitumikia Simba kwa mafanikio makubwa hivyo wachezaji wengine wanapaswa kuingia mfano wake.


Phiri aliiambia BOIPLUS kuwa tangu atue Simba kwa nyakati tofauti Mgosi alionyesha uwezo wa juu na ndio maana alipata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Motema Pembe ya DR Congo.

"Natamani kuchukuwa wachezaji kutoka Tanzania kuja kucheza huku ila nataka mchezaji nitakayempata kiwango chake kiwe kama cha Mgosi wa miaka ile ya 2010, Mgosi alitusaidia sana, alifunga mabao bora kabisa.


"Kuna nafasi lakini sidhani kama Watanzania watakubali kuja kucheza huku ingawa pia kuna maslahi mazuri. Nimewafuatilia wachezaji wa Simba wanaofunga sana sasa hivi Shiza na Mzamiru, nimeona ni wadogo wakijitunza watafika mbali kwani mafanikio yao yameonekana mapema, hivi Simba wanaweza kuwaachia kweli," alisema kocha huyo kwa kuhoji.

Phiri pia aliwashauri viongozi wa Simba kuendelea kusajili wachezaji wenye umri mdogo ambao watawasaidia kwa muda mrefu kuliko kuendelea kuwa na wachezaji ambao umri wao ni mkubwa.

"Viongozi wa Simba wana mipango mizuri ila kwa hapo walipofikia sasa hawapaswi kuwa na wachezaji wenye umri mkubwa, Mgosi alifanya jambo jema kustaafu maana asingefunga tena kwani tayari damu changa ipo pale isingekuwa rahisi kukimbizana nayo," alisema Phiri.

Post a Comment

 
Top