BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari kagoma, Dar
MAELFU ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wamejitokeza kumzika aliyekuwa Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Thomas Mashali aliyefariki juzi, mazishi yamefanyika kwenye makaburi ya Kinondoni.

Mazishi hayo yalitanguliwa na misa ya kumuombea iliyofanyika kwenye kanisa la Parokia Mtakatifu Karoli Lwanga lililopo Tandale Sokoni kabla ya kupelekwa viwanja vya Leaders ambapo ndugu jamaa marafiki pamoja na wadau wa ngumi walipata nafasi ya kutoa salamu za mwisho.

Mashali aliuawa na watu wasiojulikana usiku wa Oktoba 31 maeneo ya Kimara Bonyokwa na kuacha pengo kubwa katika tasnia ya ngumi kutokana na umri wake ambao bado alikuwa na uwezo wa kucheza zaidi ya miaka 10 ijayo.Bondia mwenzake Mada Maugo alimwelezea Mashali kama Bondia mwenye kipaji cha hali ya juu ambaye alikuwa akimpa upinzani mkubwa ulingoni na kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa katika Tasnia ya Masumbwi nchini.

Kwa upande wa Fransis Cheka alisema "Tanzania imepata pengo kubwa kwenye tasnia ya masumbwi, Mashali alikuwa anakuja vizuri sana ametupa changamoto kubwa ulingoni lakini ndiyo hivyo kazi ya Mungu haina makosa."

Rais wa Oganizesheni ya Ngumi za kulipwa nchini (TPBO) Yassin Abdallah 'Ustadhi' alisema Bondia huyo ameondoka huku akiacha alama kwa Taifa na kuwataka mabondia wengine kufuata nyayo zake lakini akiwaasa kuishi vizuri na watu kwenye Jamii zao.

Mashali ameacha mke na Watoto saba, Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahala pema peponi, Amin.

Post a Comment

 
Top